Mbali na mateka, HAMAS wana turufu nyingine hizi
Wakati vyombo vya habari vya Israel vikijaribu kuonesha suala la mateka kama kitu pekee ya mashinikizo ilicho nacho Hamas, mchambuzi mmoja wa Jordan ameionya kwamba Hamas inaweza kuvuruga mlingano huo wakati wowote kwa kutumia turufu nyingine kadhaa tofauti za kimkakati.
Shirika la Habari la Fars limenukuu Bassam Rubin, Brigedia Jenerali mstaafu wa Jordan ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kijeshi akiandika katika makala iliyochapishwa na gazeti la Rai al-Youm kwamba, utawala wa Kizayuni umetambua vyema kuwa haujaweza kuishinda Ghaza licha ya kufanya mashambulizi ya kikatili mno kuwahi kushuhudiwa kama ambavyo pia Wazayuni wanatambua kwamba muqawama bado una turufu nyingi, moja ya turufu zake hizo ni nguvu za kijeshi.
Silaha na makombora za Hamas yameendelea kubakia mikononi mwa wanamapambano wa Palestina licha ya kuzingirwa kila upande na kuripuliwa maeneo ya Ghaza usiku na mchana. Lakini silaha za HAMAS na za Muqawama zinawanyima usingizi Wazayuni.
Turufu nyingine ya HAMAS ni uungaji mkono wa kimataifa. Kila maandamano katika miji mikuu na kila kaulimbiu dhidi ya utawala wa Kizayuni ni kibao cha uso wa serikali dhaifu na tete ya Israel. Kwa kweli Israel ndiyo iliyotengwa na ndiyo inayolaaniwa kote dunani, si HAMAS.
Kwa mujibu wa mchambuzi huo wa Jordan, turufu ya tatu ya HAMAS mbali na mateka, ni jinsi kambi ya Muqawama ilivyoshikamana kwenye eneo hili. Muqawama ni kambi imara ambayo mizizi yake imetokea Tehran hadi Sanaa. Kambi hiyo haitoi vitisho vya maneno bali vitendo ndiyo sifa yake, na hilo ni pigo kwa utawala wa Kizayuni na wafuasi wake.
Aidha amesema, hiyo ni mifano tu ya turufu nyingi iliyozo nazo HAMAS, na kwamba utawala wa Kizayuni unatambua kuwa, jaribio lolote la hadaa litakabiliwa na majibu makali sana. Muqawama hauna turufu chache za mashinikizo, bali una turufu nyingine mikononi mwake ikiwemo hii ya nne ambayo ni imani thabiti ya Mwenyezi Mungu ambayo inaufanya Muqawama uzidi kuwa imara hasa kwa kutambua kwamba, adui haelewi lugha nyingine isipokuwa kutumia nguvu.