Uhispania kuiburuza Israel ICC kwa kunyanyasa wanaharakati wa msafara wa Sumud
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uhispania, Fernando Grande-Marlaska amesema kuwa, hatua za kisheria huenda zikachukuliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya Israel baada ya utawala wa Kizayuni kuvamia raia wa Uhispania waliokuwemo kwenye msafara wa Sumud au Global Sumud Flotilla uliokuwa unajaribu kuwafikishia msaada wananchi wa Ghaza.
"Nina wasiwasi kama waziri, na nina wasiwasi kama raia wa Uhispania na kama mwanadamu, kuhusu ukiukwaji wowote wa haki ya kimsingi za binadamu. Lakini kwa hilo, kuna njia za kisheria;: Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na pia mahakama za Uhispania zinazohusiana na raia wa nchi za kigeni," amesema Marlaska katika mahojiano na kituo cha televisheni cha umma cha TVE.
Marlaska pia amesisitiza kwamba msafara wa Sumud ulikuwa unaendesha kazi zake chini ya sheria ya kimataifa ya jinai, kama inavyofafanuliwa na mikataba ya wazi na inayotambuliwa pia ndani ya mfumo wa kisheria wa kitaifa.
Marlaska amebainisha kuwa, kipaumbele cha kwanza ni kwa wanachama 28 wa mwisho wa msafara wa Sumud kurejea Uhispania "salama usalimini."
Amesisitiza kwamba serikali ya Uhispania inachukua hatua katika kesi hiyo, itafika mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ili kutetea haki za kimsingi na uhuru wa umma wa raia wa Uhispania na raia wa nchi nyingine.
Matamshi hayo yanakuja wakati wanaharakati hao wa msafara wa Sumud wa kupambana na mzingiro wa Ghaza walivamiwa na wanajeshi wa Israel huku kukiwa na kesi nyingi za unyanyasaji dhidi yao.