Ripoti: Asilimia 90 ya miundombinu ya Gaza imeharibiwa
Asilimia 90 ya miundombinu ya Gaza imeharibiwa kabisa baaada ya vita vya miaka miwili vilivyoanzishwa na utawala ghasibu wa Israel.
Ofisi ya Habari ya Serikali katika Ukanda wa Gaza imechapisha ripoti inayoelezea viwango vya kutisha vya uharibifu na maafa ya kibinadamu yaliyosababishwa na uvamizi wa utawala dhalimu wa Israel katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa Kanali ya televisheni ya Al-Mayadeen, ofisi hiyo imetangaza kwamba licha ya uharibifu mkubwa na hali ngumu sana, timu za serikali na wizara zimefanya zaidi ya misheni 5,000 muhimu katika Ukanda wa Gaza katika masaa 24 iliyopita.
Kati ya hizo, zaidi ya misheni 2,000 zilijitolea kwa ajili ya huduma za matibabu, ikijumuisha upasuaji wa dharura na misaada kwa waliojeruhiwa na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
Katika sehemu nyingine ya ripoti hiyo, Ofisi ya Habari ya Ukanda wa Gaza imesisitiza kuwa, hujuma za utawala huo ghasibu zimesababisha uharibifu mkubwa, unaofunika zaidi ya asilimia 90 ya miundombinu yote ya kiraia katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatua hizi pamoja na uharibifu mkubwa zimesababisha uharibifu wa makazi zaidi ya 300,000, na kwa sababu hiyo, wakazi milioni mbili wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao kwa nguvu.
Wakati huo huo, Jumuiya ya Magereza ya Kizayuni imepokea amri ya kuwaachilia huru mateka wa Palestina kama vinavyosema vipengee vya makubaliano ya kusimamisha vita yanayojumuisha kuachiliwa huru mateka.
Ripoti zinasema, mateka wa Palestina wataachiliwa huru kutoka magereza matano ya Israel na tayari mateka hao wameashaanza kutolewa kwenye jela hizo na kupelekea maeneo maalumu ya kuwaachilia huru.