Umoja wa Mataifa: Wayemen milioni 17 wanakabiliwa na njaa kali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133326-umoja_wa_mataifa_wayemen_milioni_17_wanakabiliwa_na_njaa_kali
Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake ya hivi punde kwamba raia milioni 17 wa Yemen wanakabiliwa na njaa kali, na idadi hii inatarajiwa kuongezeka.
(last modified 2025-11-18T10:49:27+00:00 )
Nov 18, 2025 10:49 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Wayemeni milioni 17 wanakabiliwa na njaa kali
    Umoja wa Mataifa: Wayemeni milioni 17 wanakabiliwa na njaa kali

Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake ya hivi punde kwamba raia milioni 17 wa Yemen wanakabiliwa na njaa kali, na idadi hii inatarajiwa kuongezeka.

Akiwasilisha ripoti kuhusu ukosefu wa usalama wa chakula uliosababishwa na vita nchini Yemen, Joyce Msuya, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, alisema uharibifu wa miundombinu nchini humo umetatiza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, na migogoro inayoendelea inasababisha watu kuhama makazi yao na kuzidisha mdororo wa kiuchumi.

Msuya aliongeza: "Watu milioni 17 bado wanakabiliwa na njaa kali nchini Yemen, na makadirio yanaonyesha kuwa watu wengine milioni wataongezwa kwenye idadi hii."

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema ukosefu wa usalama wa chakula nchini Yemen ni "mfano wa wazi wa uhusiano kati ya vurugu na njaa." Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yanasababisha kutelekezwa kwa mashamba, kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji wa chakula, kupanda kwa bei na uharibifu wa maisha.

Benki ya Dunia pia ilitahadharisha juu ya kuenea kwa mzozo wa njaa nchini Yemen, ikisema kuwa zaidi ya asilimia 60 ya familia zinakabiliwa na shida katika kupata chakula, na hali hii inawafanya wengi wao kuelekea kwenye machaguzi magumu kama vile kuwa ombaomba.

Wakati huo huo, ripoti mpya ya pamoja ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) la na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) metahadharisha kuwa, hali ya ukosefu wa usalama wa chakula inazidi kuwa mbaya katika maeneo 16 yenye janga la njaa duniani, huku mamilioni ya watu wakiwa katika hatari ya kupatwa na janga hilo katika kipindi cha kati ya Novemba 2025 na Mei 2026.