Hamas yakemea mauaji na mateso ya wafungwa Wapalestina magerezani Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133660-hamas_yakemea_mauaji_na_mateso_ya_wafungwa_wapalestina_magerezani_israel
Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina (Hamas) imelaani vikali mauaji ya makusudi na mateso ya Wapalestina walioko katika magereza ya kuogofya ya utawala haramu wa Israel, ikiyataja kama “uhalifu kamili wa kivita” na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti.
(last modified 2025-11-27T12:19:58+00:00 )
Nov 27, 2025 12:19 UTC
  • Wafungwa Wapalestina magerezani Israel
    Wafungwa Wapalestina magerezani Israel

Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina (Hamas) imelaani vikali mauaji ya makusudi na mateso ya Wapalestina walioko katika magereza ya kuogofya ya utawala haramu wa Israel, ikiyataja kama “uhalifu kamili wa kivita” na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti.

Katika taarifa yake ya Alhamisi, Hamas imesema kuwa utawala wa Kizayuni umegeuza magereza yake kuwa vituo vya mateso na mauaji ya moja kwa moja dhidi ya wafungwa wa Kipalestina.

Tangu Israeli ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 2023, makumi ya wafungwa Wapalestina wameuawa na wengine wengi kuteswa kwa ukatili. Hamas imeripoti kuwa angalau Wapalestina 94 wamefariki wakiwa kizuizini tangu Oktoba 2023, huku mashirika ya haki za binadamu na manusura wakitoa ushahidi wa unyama wa kutisha, ikiwemo kupigwa vibaya, kumwagiwa maji ya moto, kushambuliwa na mbwa, ukatili wa kingono, pamoja na kunyimwa chakula, usingizi na huduma za afya.

Hamas imesema kuwa magereza haya yamegeuzwa kuwa viwanja vya mauaji ya moja kwa moja ili kuangamiza watu wao, na ikasisitiza kuwa vitendo hivyo ni uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu vinavyofichua asili ya kikatili ya utawala wa Kizayuni. Harakati hiyo imeutaka Umoja wa Mataifa, mashirika ya haki za binadamu, na jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Israel kusitisha ukatili huu na kuhakikisha haki za wafungwa zinalindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Kwa sasa, inakadiriwa kuwa zaidi ya Wapalestina 10,000, wakiwemo wanawake na watoto, wanashikiliwa katika magereza hatari ya Israel.

Aidha, tangu ianzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza Oktoba 2023, Israel imeua takribani Wapalestina 70,000 na kuwajeruhi zaidi ya 170,000 katika eneo hilo ambalo bado liko chini ya mazingiro.