Ma'ariv: Jeshi la Israel limechoka baada ya miaka miwili ya vita
Chombo cha habari cha Kizayuni kimefichua katika ripoti yake kwamba baada ya miaka miwili na miezi miwili ya vita vikali katika pande saba, jeshi la Israel limechakaa, maafisa wake wamechoka, na wanajeshi wana ndoto ya kurudi majumbani mwao.
Gazeti la Ma'ariv limeeleza katika ripoti yake kwamba jeshi la Israel linakabiliwa na uhaba wa karibu wanajeshi 12,000, ambapo 9,000 ni wanajeshi wa kivita na 3,000 ni wanajeshi wa usaidizi.
Gazeti hilo la Kizayuni limefichua kuwa: "Kwa maneno mengine, jeshi la Israel sasa lina uhaba wa askari, na imepangwa kuwa askari wa akiba wataitwa kwa siku 60 mwaka wa 2026."
Ma'ariv pia imeandika kwamba sheria ya kuandikisha watu kwa lazima jeshini iliyopendekezwa bungeni haitakidhi mahitaji ya jeshi la utawala huo, na baadhi ya maafisa wanasema, pendekezo hilo ni ujanja wa kisiasa.
Maafisa wa Israel wanakiri kuwa wanajeshi wasiopungua 900 wa utawala huo wameuawa huko Gaza na wengine 6,210 wamejeruhiwa. Hata hivyo wanachambuzi wa mambo wanasema, idadi ya wanajeshi wa Israel waliouawa tangu baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa ni kubwa zaidi kuliko ile inayitangazwa rasmi.
Jeshi la Israel pia lina historia ya kuficha idadi ya askari wake wanaouawa vitani ili kudumisha motisha jeshini na kuonyesha umma wa Israel kwamba eti wanashinda vita dhidi ya wapigania ukombozi wa Palestina.