Amnesty International yaonya kuhusiana na hali ya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134014-amnesty_international_yaonya_kuhusiana_na_hali_ya_gaza
Katibu Mkuu wa Amnesty International sambamba na kueleza wasi wasi wake mkubwa kuhusu hali ya Gaza amesisitiza kuwa: Jamii ya kimataifa imejitenga kuiwajibisha Israel na haiangazii na kuzingatia tena hali ya Gaza.
(last modified 2025-12-07T06:49:37+00:00 )
Dec 07, 2025 06:49 UTC
  • Amnesty International yaonya kuhusiana na hali ya Gaza

Katibu Mkuu wa Amnesty International sambamba na kueleza wasi wasi wake mkubwa kuhusu hali ya Gaza amesisitiza kuwa: Jamii ya kimataifa imejitenga kuiwajibisha Israel na haiangazii na kuzingatia tena hali ya Gaza.

Agnes Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International amesema hayo katika mahojiano na Televisheni ya Al-Arabi na kuelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali ya Gaza na kutangaza kwamba mauaji ya kimbari yanaendelea katika eneo hilo.

Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International ametaka kesi mpya zifunguliwe dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili haki ipatikane kwa uhalifu unaoweza kutokea huko Gaza.

Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imezitaka mahakama za kimataifa na vyombo husika kuwafungulia mashtaka wale waliohusika wa uhalifu wa kivita baada ya uchunguzi kufichua kwamba wanajeshi wa Israel waliteketeza miili ya Wapalestina waliokuwa katika safu za kupokea misaada na kuizika katika makaburi yasiyo na kina huko Gaza.

Licha ya kusitishwa mapigano huko Gaza, lakini bado mateso ya njaa na ukosefu wa usalama na utulivu wa nafsi yanaendelea kuzisumbua familia za Wapalestina. Foleni ndefu za watu wenye njaa wanaosubiri kupata angalau mlo mmoja kwa siku zinaendelea kuonekana katika pembe mbalimbali za ukanda huo huku jeshi katili la Israeli likiendeleza mashambulizi ya mara kwa mara na kuzuia kuwafikia misaada wananchi hao wasio na ulinzi.

Ripoti kutoka Gaza zinaonyesha kuwa, mistari mirefu inaonekana kila siku kwenye vituo vya kugawa chakula cha hisani kwa matumaini ya kupokea angalau mlo mmoja kwa siku, huku jeshi la Israeli likiendelea kuzuia malori ya misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.