Watoto wa Gaza walilipa gharama kubwa mwaka uliomalizika majuzi wa 2025
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135068-watoto_wa_gaza_walilipa_gharama_kubwa_mwaka_uliomalizika_majuzi_wa_2025
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watoto wa Gaza walilipa gharama kubwa mwaka uliomalizika wa 2025 kutokana na vita na mzingiro wa utawala wa Israel dhidi ya Ukanda huo.
(last modified 2026-01-03T16:16:12+00:00 )
Jan 03, 2026 12:04 UTC
  • Watoto wa Gaza walilipa gharama kubwa mwaka uliomalizika majuzi wa 2025
    Watoto wa Gaza walilipa gharama kubwa mwaka uliomalizika majuzi wa 2025

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watoto wa Gaza walilipa gharama kubwa mwaka uliomalizika wa 2025 kutokana na vita na mzingiro wa utawala wa Israel dhidi ya Ukanda huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa, tangazo la njaa katika baadhi ya maeneo ya Mji wa Gaza katika majira ya joto ya 2025 kutokana na vita, mzingiro, na kuzuia kuwasili kwa misaada ilikuwa sehemu ya gharama hizo ambazo zimechukua roho za maelfu ya watoto wa Kipalestina.

UNICEF imetangaza kwamba watoto huko Gaza wanakabiliwa na hatari ya njaa, magonjwa na vifo kutokana na vita vinavyoendelea.

Taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa kinachoendelea Gaza si maafa na majanga ya kimaumbile, bali ni matokeo ya moja kwa moja ya vita na mzingiro.

UNICEF imekosoa utendaji wa jamii ya kimataifa katika Ukanda wa Gaza na kuongeza: "dunia imeshindwa na tumewaangusha watoto wa Gaza ambao wanaendelea kufa kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika wakati wa majira ya baridi." Takwimu zinaonyesha kuwa, watoto 82 wamefariki dunia katika Ukanda wa Gaza tangu usitishaji vita uanze kutekelezwa, jambo ambalo linashangaza na lazima likomeshwe.

Wakati huo huo, imeelezwa kuwa, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huko Gaza hadi hivi sasa zimeshaharibu asilimia 90 ya mahema ya wakimbizi wa ukanda huo tena wakati huu wa kukaribia kuingia kwenye msimu wa baridi kali.