Hamas: Quds na Msikiti wa Al-Aqsa ndio utambulisho wa Palestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kwamba uvamizi wa walowezi wa Kizayuni na kufanya "maandamano ya bendera" huko Quds (Jerusalem) na Msikiti wa Al-Aqsa ni majaribio yaliyoshindwa ya kutaka kubadilisha utambulisho wa ardhi takatifu ya Palestina.
Taarifa hiyo ya Hamas imetolewa katika kukabiliana na shambulio la maelfu ya walowezi wa Israel katika mji wa kale wa Quds (Jerusalem), ulilotekwa na kukaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya Waarabu na utawala huo haramu mwaka 1967.
Harakati ya Hamas imesisitiza katika taarifa yake kwamba haijalishi ni kwa kiasi gani wavamizi magaidi wanaongeza nguvu ya vitendo vyao vya ukatili na mashambulizi dhidi ya wakazi wa Quds, hawataweza kamwe kuondoa hadhi na nafasi ya Quds na Msikiti wa Al-Aqsa katika nyoni za watoto wa taifa la Palestina au kudhoofisha azma ya kutetea matakatifu yao.
Hamas imeongeza: "Muqawama wa Palestina utabaki kuwa mwaminifu kwa ahadi yake ya kutetea Msikiti wa Al-Aqsa na kulinda taifa la Palestina, ardhi na maeneo matakatifu, na dira yake daima itaelekeza kwenye ukombozi na kutoka kwenye makucha ya uvamizi bila kujali kiasi cha gharama, ukatili na njama za Wazayuni."
Muqawama wa Palestina umehitimisha kwa kusisitiza kwamba: "Tunatoa wito kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kutimiza majukumu yao ya kihistoria na kidini kuhusu Quds Tukufu na Msikiti wa Al-Aqsa. Pia tunawaomba wafanye juhudi zao zote za kukomesha uchokozi unaoendelea, kuvuruga mipango ya wavamizi, na kutoa mashinikizo kwa adui kwa njia zote na katika ngazi mbalimbali."
Maandamano ya kila mwaka ya Wazayuni katika mji mtakatifu wa Quds maarufu kama "Flag March" mara nyingi huambatana na nyimbo za kibaguzi na vurugu dhidi ya wakazi na biashara za Wapalestina.