Makumi wauawa katika shambulio la bomu lililolenga kituo cha treni Pakistani
-
Maafisa wa usalama wakichunguza eneo la mlipuko katika kituo cha treni huko Quetta, Pakistan mnamo Mei 24, 2026
Shambulio la kigaidi katika kituo cha treni katika mji mkuu wa jimbo la Balochistan nchini Pakistani limesababisha vifo vya watu 24 na kujeruhiwa wengine wengi.
Mhusika wa shambulio hilo, ambaye alikufa katika mlipuko huo, alilipua bomu katika kituo cha treni cha Quetta siku ya Jumamosi.
Maafisa wa serikali ya Pakistan wanasema kwa uchache watu 24, wakiwemo wanajeshi 12 na wafanyakazi sita wa reli, wameuawa na wengine wapatao 50, baadhi wakiwa katika hali mbaya, wamejeruhiwa.
Hamza Shafqaat, msimamizi mkuu wa serikali katika eneo hilo, amesema shambulio hilo la kigaidi lilitokea wakati abiria walipokuwa wakisubiri treni iliyokuwa ikielekea katika mji wa Rawalpindi.
Milio mikubwa ya risasi ilisikika baada ya shambulio hilo. Picha za CCTV zilionyesha uharibifu mkubwa wa kituo cha eneo la mlipuko na mizigo ya abiria iliyoachwa nyuma.
Kundi la Balochistan’s Liberation Army (BLA) limedai kuhusika na shambulio hilo.
Islamabad inakabiliwa na upinzani wa muda mrefu wa makundi ya wanamgambo yanaotaka kujitenga eneo la kusini magharibi mwa Pakistan. Awali, vikosi vya jeshi vya Pakistan vilifanya mashambulizi dhidi ya "vituo" vya waasi katika eneo hilo.
Shambulio la Jumamosi linafanyika huku Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, Jenerali Syed Asim Munir akiondoka Tehran baada ya kukamilisha ziara rasmi ya upatanishi ili kujadili jinsi ya kuendeleza mashauriano unaolenga kurejesha amani na utulivu katika eneo la Maghariibi mwa Asia na kufikia makubaliano kamili kati ya Iran na Marekani.