Afisa wa zamani wa Kizayuni: Hatimaye tutatoroka Lebanon kwa madhila
-
Wanajeshi wa Israel
Mkuu wa zamani wa Kamati ya Usalama na Mahusiano ya Kigeni katika Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel amesema kwamba utawala huo hatimaye utatoroka Lebanon kwa madhila na kushindwa.
Ofer Shallah amesema kwamba shughuli za vikosi vya jeshi la utawala huo nchini Lebanon hazijatimiza lengo lolote.
Amesisitiza kuwa: "Fikra ya kuanzisha ukanda wa usalama kusini mwa Lebanon ni kichocheo cha maafa na hakutafanikisha chochote, na tutapoteza wanajeshi wetu na hatimaye tutakimbia Lebanon tukiwa tumeshindwa kabisa, kama ilivyokuwa mwaka wa 2000."
Hapo awali, tovuti ya habari ya Wazayuni, Vala, iliwanukuu maafisa wakuu wa Israel wakisema: "Tunakabiliwa na changamoto kubwa kusini mwa Lebanon, na ni vigumu kufuatilia na kuzuia ndege zisizo na rubani za Hizbullah."
Gazeti la Wazayuni Haaretz pia limewanukuu maafisa wa jeshi waliokuwa kusini mwa Lebanon wakisema: "Hatuelewi mkakati wa makamanda wetu. Dhamira yetu ya msingi ni kuharibu nyumba katika vijiji vya Lebanon."
Gazeti la Kizayuni Israel Hayom pia limeandika, likiwanukuu maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Israel, kwamba kubakia Lebanon hakuna maana na jeshi halijapata mafanikio yoyote katika vita dhidi ya Hizbullah.