Kwa nini utawala wa Kizayuni unasisitiza kuendeleza vita huko Lebanon?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138742-kwa_nini_utawala_wa_kizayuni_unasisitiza_kuendeleza_vita_huko_lebanon
Moja ya vikwazo muhimu katika mazungumzo ya Iran na Marekani ni sisitizo la utawala wa Kizayuni wa Israel la kuondolewa medani ya vita vya Lebanon kwenye mazungumzo hayo na kuendeleza vita dhidi ya harakati ya Hizbullah. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa moja ya masharti muhimu ya kufikiwa mapatano na Marekani ni kusimamishwa kikamilifu vita katika ngome zote za mhimili wa muqawama na hasa nchini Lebanon.
(last modified 2026-05-30T07:07:02+00:00 )
May 30, 2026 07:00 UTC
  • Kwa nini utawala wa Kizayuni unasisitiza kuendeleza vita huko Lebanon?

Moja ya vikwazo muhimu katika mazungumzo ya Iran na Marekani ni sisitizo la utawala wa Kizayuni wa Israel la kuondolewa medani ya vita vya Lebanon kwenye mazungumzo hayo na kuendeleza vita dhidi ya harakati ya Hizbullah. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa moja ya masharti muhimu ya kufikiwa mapatano na Marekani ni kusimamishwa kikamilifu vita katika ngome zote za mhimili wa muqawama na hasa nchini Lebanon.

Swali muhimu ni kuwa je, kwa nini utawala wa Kizayuni unasisitiza kuendeleza vita huko Lebanon?

Jibu la swali hili linapaswa kuchunguzwa katika viwango vitatu vya Lebanon na Israel, kikanda na kimataifa.

Kuhusu Lebanon, utawala wa Kizayuni unaamini kuwa, nafasi ya hivi sasa ya Hizbullah katika muundo wa madaraka ni tofauti kabisa na ilivyokuwa huko nyuma. Kutokana na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Lebanon, hivi sasa baadhi ya nyadhifa muhimu za madaraka nchini humo zinashikiliwa na watu walio mbali kifikra na muqawama na ambao wakati huo huo wanafungamana na siasa za Marekani na utawala wa Kizayuni kuhusu suala la kupokonywa silaha Hizbullah. Kwa hiyo, Wazayuni wanaamini kuwa Hizbullah hivi sasa iko katika nafasi dhaifu na inayoweza kutumiwa vibaya na utawala huo katika kufikia malengo yake haramu katika ardhi ya Lebanon. Kwa hivyo, kwa kuendeleza mashambulizi dhidi ya Hizbullah, Wazayuni wanajaribu kushadidisha mifarakano ya ndani nchini humo na kuidhihirisha Hizbullah kama tishio kwa maslahi na usalama wa taifa la Lebanon.

Kadhalika, baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu, ambalo liko chini ya mashinikizo makubwa ya kisiasa na kimahakama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kutoka kwa wakosoaji wake na maoni ya waliowengi, linajaribu kudumisha hali ya vita kwa maslahi ya kisiasa ya baraza la Netanyahu kwa kuendeleza vita dhidi ya Hizbullah, kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, kujaribu kuonyesha kuwa linachukua maamuzi huru ya vita dhidi ya Hizbullah mbali na mashinikizo ya ya Washington.

Katika ngazi ya kieneo, mtazamo wa utawala wa Kizayuni ni kwamba kwa kuendeleza vita dhidi ya Hizbullah, utakuwa unaendelea kutoa mapigo dhidi ya Hizbullah hususan na kwa mhimili wa muqawama kwa ujumla. Mapigo haya yanatimia kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Hizbullah na kuua makamanda wake. Lengo kuu la utawala wa Kizayuni ni kudhoofisha mhimili wa muqawama katika ngazi ya kieneo, na bila shaka Hizbullah ni miongoni mwa wahusika wakuu katika mhimili huu, ambapo pia ipo karibu na mipaka ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Aidha katika ngazi ya kieneo, utawala wa Kizayuni unafuatilia kuibua mpasuko kati ya wachezaji muhimu wa mhimili wa muqawama na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama lengo lake kuu. Kwa kuendeleza mashambulio dhidi ya Hizbullah, utawala huo ghasibu unalenga kufikia lengo kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kuwalinda washirika wake wa kieneo na kwamba inataka tu kujidhaminia usalama wake yenyewe bila kusimamisha vita dhidi ya washirika wake. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kubatilisha madai hayo ya utawala wa Kizayuni kwa kusisitiza ulazima wa kuhitimishwa vita katika ngome zote za mapigano.

Katika ngazi ya kimataifa, utawala wa Kizayuni unajaribu kuzuia kufikiwa makubaliano kati ya Iran na Marekani kwa kushadidisha mashambulio katika maeneo ya kusini mwa Lebanon. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kusimamishwa mapigano katika ngome zote dhidi ya mhimili wa muqawama kama moja ya masharti ya kufikiwa makubaliano na Marekani. Utawala wa Kizayuni ambao unaona kuwa makubaliano ya Iran na Marekani ni kwa madhara yake, inaishinikiza Marekani iendeleze vita na Iran, huku ikijaribu kuvuruga mazungumzo hayo kwa kuendeleza vita dhidi ya Hizbullah.

Nukta ya mwisho ni kwamba, hata kama utawala wa Kizayuni utalemewa na mashinikizo ya Marekani na hatimaye kukubali kusimamisha vita dhidi ya Hizbullah, lakini ni wazi kuwa historia ya mfumo wa kitabia wa utawala huo inausaliti na hivyo hauwezi kuaminika katika kutekeleza ahadi zake za kusitishaji vita na uchokozi katika eneo na hasa dhidi ya Hizbullah. Utawala wa Kizayuni haujaheshimu makubaliano yoyote tangu kuasisiwa kwake mwaka 1948 na daima umekuwa ukikiuka makubaliano ya kimataifa. Kuhusiana na suala hilo hata mwakilishi wake katika Umoja wa Mataifa alichanachana hadharani Hati ya Umoja wa Mataifa mbele ya wawakilishi wa nchi 194 na kutoona aibu yoyote katika kutoa wito wa kufungwa Umoja huo.