Je, Israel inafuatilia malengo gani katika kuzidisha vita nchini Lebanon?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138856-je_israel_inafuatilia_malengo_gani_katika_kuzidisha_vita_nchini_lebanon
Utawala wa Kizayuni unaendelea kushambulia Lebanon ambapo katika siku za hivi karibuni ulikuwa umetishia kuushambulia mtaa wa Dhahiyah kusini mwa Beirut na kutaka watu wahame kutoka eneo hilo. Swali muhimu ni je, kwa nini utawala wa Kizayuni unataka kushadidisha mgogoro na vita nchini Lebanon?
(last modified 2026-06-03T12:51:48+00:00 )
Jun 03, 2026 12:13 UTC
  • Je, Israel inafuatilia malengo gani katika kuzidisha vita nchini Lebanon?

Utawala wa Kizayuni unaendelea kushambulia Lebanon ambapo katika siku za hivi karibuni ulikuwa umetishia kuushambulia mtaa wa Dhahiyah kusini mwa Beirut na kutaka watu wahame kutoka eneo hilo. Swali muhimu ni je, kwa nini utawala wa Kizayuni unataka kushadidisha mgogoro na vita nchini Lebanon?

Moja ya sababu muhimu zaidi za hatua za kichokozi za utawala wa Kizayuni katika kushadidisha vita na jinia dhidi ya Hizbullah ya Lebanon ni kwamba utawala huo hauifasiri Hizbullah katika fremu ya Lebanon, bali katika fremu ya mhimili wa muqawama, na kwa maneno mengine, ni harakati inayovuka mipaka ya Lebanon. Kwa hivyo, fikra ya utawala wa Kizayuni ni kwamba unataka kuudhoofisha mhimili wa muqawama kupitia mashambulizi makali dhidi ya Hizbullah huko Lebanon.

Sababu nyingine kuu ya utawala wa Kizayuni kushadidisha vita na mashambulizi dhidi ya Lebanon ni kuhusiana na hali ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu. Hivi sasa huko Lebanon baadhi ya watu walioko madarakani wanashirikiana kwa karibu na utawala wa Kizayuni katika kadhia ya kupokonywa silaha Hizbullah, na muhimu zaidi ni kwamba hawaonyeshi hisia zozote dhidi ya Utawala wa Kizayuni  kutokana na mauaji ya kinyama unayoyafanya dhidi ya watu wa Lebanon. Kwa hivyo, Tel Aviv inachukulia hali ya sasa ya uongozi dhaifu wa Lebanon kama fursa ya kutoa pigo kubwa zaidi la kijeshi dhidi ya Hizbullah. Wazayuni wanaamini kuwa Hizbullah iko katika hali dhaifu ambapo wanaweza kunufaika nayo kwa maslahi yao kwa sababu serikali ya Lebanon nayo inajaribu kutoa mashinikizo dhidi ya harakati hiyo ya muqawama.

Sababu nyingine ya utawala wa Kizayuni kushadidisha vita na mgogoro dhidi ya Hizbullah ya Lebanon ni kuhusiana na mazungumzo yanayoendelea kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani. Moja ya masharti muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kufikia mapatano na Marekani ni kusimamishwa vita katika medani zote za vita hususan nchini Lebanon. Kwa kushadidisha mashambulizi dhidi ya Lebanon, utawala wa Kizayuni unajaribu kuathiri mazungumzo kati ya Iran na Marekani na kuzizuia pande hizo kufikia makubaliano. Kwa hakika utawala wa Kizayuni siku zote umekuwa chanzo cha kuvuruga mazungumzo kati ya Iran na Marekani na unaendelea kutekeleza nafasi hiyo hivi sasa.

Sababu nyingine ni kuwa, utawala wa Kizayuni unataka kuteka maeneo mengi zaidi ya Lebanon ili kuyageuza kuwa chombo cha mashinikizo dhidi ya Lebanon kabla ya kusimamishwa vita katika ngome zote, ambalo ni moja ya matakwa makuu ya Iran katika uwanja huo. Utawala wa Kizayuni unaona kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa makubaliano kati ya Iran na Marekani, jambo ambalo huenda likapelekea kusitishwa mapigano nchini Lebanon, kabla ya Tel Aviv kufikia lengo lake kuu la kupokonywa silaha Hizbullah.

Ni sababu hizo ndizo zimeufanya utawala wa Kizayuni kushadidisha vita dhidi ya Lebanon katika mazingira ya sasa. Bila shaka kufuatia onyo kali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba kuendelea mashambulizi dhidi ya Lebanon kutakabiliwa na jibu kali la Iran, utawala wa Kizayuni hatimaye umesimamisha mashambulizi dhidi ya mtaa wa Dhahiya kwa mashinikizo ya Marekani.