Mamia ya Wapalestina wametekwa nyara na wanajeshi wa Israel mwezi uliopita
Taasisi na duru mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya mateka wa Kipalestina wamesema kuwa, Wapalestina 516 wametekwa nyara na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi uliopita katika mikoa mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina, Kamati ya Masuala ya Mateka na Wapalestina Wanaoachiliwa Huru, Asasi ya Mateka wa Kipalestina, Taasisi ya Kuwasaidia mateka ya "al Dhwamir" na kituo cha haki za binadamu cha al Mizan zimetoa ripoti ya pamoja na sambamba na kuthibitisha habari ya kutekwa nyara mamia ya Wapalestina katika kipindi cha mwezi ulioisha wa Agosti zimesema kuwa, 73 kati ya Wapalestina hao waliotekwa nyara ni watoto wadogo, 10 ni wanawake na wawili na visichana vidogo.
Habari nyingine inasema kuwa, baada ya wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni kumshambulia kinyama kijana mmoja wa Kipalestina katika eneo la Tel Buyut, katikati ya mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni hiyo jana, walivamia nyumba moja katika kitongoji cha Salwan, kusini mwa Masjidul Aqswa na kumteka nyara kijana mwingine wa Kipalestina.
Vile vile wanajeshi hao wamevamia nyumba moja ya kijana wa Kipalestina na kuharibu kila kitu baada ya kumteka nyara na kumpeleka kusikojulikana.
Wanajeshi hao wamevamia pia kitiongoji cha Barqin na kumteka nyara tena Mpalestina mmoja aliyewahi kutekwa nyara huko nyuma. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi dhalimu wa Israel wamewateka nyara vijana wengine wawili wa Kipalesitna kaskaizni mwa mji wa Tulkarm na kuwapeleka kusikojulikana. Wapalestina wengine wanne wametekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika maeneo tofauti ya mji wa al Khalil.