Saudi Arabia yazidi kuwachochea maadui wa taifa la Iran
Utawala wa ukoo wa Aal Saud wa Saudi Arabia umeendelea na hatua zake za kiuadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kuzidi kuonesha uadui wake dhidi ya Iran. Katika hatua ya karibuni kabisa ya uadui huo, viongozi wa Saudia wamewafanya kuwa wageni wao rasmi watu wanaoendesha uchochezi ndani ya Iran.
Shirika la habari la Fars limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mbali na kitendo cha kiuadui cha hivi karibuni cha Turki al Faisal, mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la Saudi Arabia kushiriki katika mkutano wa genge la kigaidi la MKO lenye historia ya kufanya jinai nyingine nchini Iran, mkutano ambao ulifanyika katika viunga vya Paris Ufaransa, na kutangaza kuwa analiunga mkono kikamilifu genge hilo la kigaidi, viongozi wa Saudi Arabia wameendelea kuwaalika wahalifu wanaosakwa kujibu jinai zao dhidi ya wananchi wa Iran. Hatua hiyo ya Turki al Faisal ya kushiriki katikamkutano huo iliuingiza uadui wa Riyadh dhidi ya Iran katika hatua mpya.
Si hayo tu, lakini pia, viongozi wa Saudi Arabia wamekuwa wakifanya propaganda kubwa kwa kutumia vyombo vyao vya habari kufunika jinai za genge la kigaidi la MKO dhidi ya wananchi wa Iran.
Mbali na misaada ya kifedha inayotolewa na viongozi wa Saudia kwa wahalifu hao, hivi karibuni viongozi wa Riyadh wamewaalika wahalifu hao kutembelea Saudia na kushiriki katika ibada ya Hija ili kutumia fursa hiyo kuendesha propaganda mbaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, gazeti la Okaz la Saudia limesema, wahalifu wanaokabiliwa na tuhuma nyingi za kufanya jinai ndani ya Iran wamealikwa nchini Saudia na kutakiwa na viongozi wa Riyadh watumie vyombo vya habari kusifia usimamiaji wa Hija unaofanywa na viongozi wa utawala wa Aal Saud.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Jamal Poorkarim, mmoja wa waungaji mkono wa magenge yanayotaka kuigawa vipande vipande Iran, Reza Hossein na Naser Zehi, wauangaji mkono wa genge moja linalofanya vitendo vya uhalifu kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia katika eneo la Sistan va Baluchistan nchini Iran ni miongoni mwa wahalifu walioalikwa na utawala wa Aal Saud katika Hija ya mwaka huu.