Kufichuliwa jinai mpya za Israel dhidi ya watoto
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i15298-kufichuliwa_jinai_mpya_za_israel_dhidi_ya_watoto
Ripoti iliyochapishwa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni zimewakasirisha viongozi wa utawala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 14, 2016 03:38 UTC
  • Kufichuliwa jinai mpya za Israel dhidi ya watoto

Ripoti iliyochapishwa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni zimewakasirisha viongozi wa utawala huo.

Dan Danon Balozi wa Israel nchini Marekani ametoa radiamali yake kwa ripoti iliyotolewa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa iliyoeleza kuwa, Israel ni sababu za kuongezeka vifo vya watoto wa Kipalestina katika eneo la Ukanda wa Ghaza kwa kusema kwamba, ripoti hiyo imetayarishwa kwa ushawishi wa Wapalestina katika Umoja wa Mataifa. Danon amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutotekeleza mapendekezo yaliyowasilishwa ndani ya ripoti hiyo.  

Ombi hilo limetolewa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika hali ambayo Ban Ki-moon siku kadhaa zilizopita alipuuza ombi la kimataifa la kutaka kuuweka utawala wa Kizayuni katika orodha ya wakiukaji wa haki za binadamu licha ya ripoti nyingi zilizotolewa na taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa na jumuiya nyingine za kimataifa kuhusu mauaji ya watoto yanayofanywa na Israel.

Upuuzaji wa Umoja wa Mataifa mkabala na utawala unaotenda jinai wa Kizayuni unautia kiburi utawala huo cha kuendeleza jinai zake. Vitendo vya kibaguzi vinavyofanywa na utawala wa Israel unaowauwa watoto  vimekuwa vya kutisha na vya hatari sambamba na kukabiliwa pia na wimbi la malalamiko na hasira za walimwengu.  

Wanajeshi wa Israel wakimburuta kwa nguvu mtoto wa Kipalestina

Tangu kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina mwaka 1948, watoto wa Palestina wamekuwa wahanga wakuu wa jinai za kivita na maangamizi ya kizazi yanayofanywa na utawala wa Israel katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo dhalimu. Takwimu zilizotolewa katika muongo mmoja uliopita zinaonyesha kuwa watoto wa Kipalestina zaidi ya 1500 wameuliwa shahidi na wengine zaidi ya elfu nane pia wanashikiliwa katika jela na kwenye korokoro za utawala wa Kizayuni kwa muda sasa. 

Aidha watoto wa Kipalestina zaidi ya laki nane wanataabika kwa umaskini huku wakikabiliwa na ukosefu wa suhula za dharura na huduma za msingi kutokana na siasa za Israel za kuwashinikiza zaidi raia wa Palestina. Wakati huo huo  watoto elfu moja wa Kipalestina pia wanalazimika kufanya kazi za vibarua ili kudhamini maisha yao au ya familia zao. Utawala wa Kizayuni ambao unaongoza miongoni mwa tawala zinazokiuka na kukanyaga wazi wazi sheria za kimataifa, zinawakamata kiholela watoto wadogo wa Kipalestina, zinawahukumu na kuwafunga jela huku watoto hao wakiteswa kwa njia mbalimbali. 

Mtoto wa Kipalestina akiteswa na wanajeshi wa Israel 

Kuuliwa ovyo Wapalestina limekuwa ni jambo la kila uchao na sehemu ya utamaduni wa viongozi wapenda vita wa utawala wa Kizayuni; kiasi kwamba hakuna siku inayopita bila ya kusikia habari ya kujiri vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Wapalestina na kuuliwa raia hao na utawala wa Kizayuni khususan watoto na vijana. Miamala ya utumiaji mabavu ya utawala huo unaoikalia Quds kwa mabavu dhidi ya watoto wa Kipalestina inakinzana na sheria za kimataifa hasa kipengee cha 16 cha Azimio la Haki za Watoto ambacho kinapiga marufuku miamala ya utumiaji mabavu dhidi ya watoto.