Mwanaharakati wa kisiasa Bahrain: Saudia ndio inatoa hukumu ya kamatakamata Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i15427-mwanaharakati_wa_kisiasa_bahrain_saudia_ndio_inatoa_hukumu_ya_kamatakamata_bahrain
Mwanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain amesema kuwa, idara ya ujasusi ya Saudia ndio inayotoa hukumu ya nani akamatwe huko nchini Bahrain.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 16, 2016 03:31 UTC
  • Mwanaharakati wa kisiasa Bahrain: Saudia ndio inatoa hukumu ya kamatakamata Bahrain

Mwanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain amesema kuwa, idara ya ujasusi ya Saudia ndio inayotoa hukumu ya nani akamatwe huko nchini Bahrain.

Adel al-Gharif ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la FARS na kubainisha kwamba jela za utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain zimejaa watu wasio na hatia wakiwamo watoto 35 na wanawake 195 na kwamba, wanawake na watoto wa Bahrain hawajasalimika kutokana na dhulma na ukandamizaji wa utawala wa kidikteta wa nchi hiyo. Mwanasiasa huyo ameongeza kuwa, makumi ya watu hao wanaoshikiliwa katika jela hizo, wanaumwa maradhi mbalimbali kutokana na kunyimwa huduma na kwamba hupoteza maisha wanapoachiliwa huru.

Mmoja wa raia aliyeuawa na maafisa usalama wa Bahrain

Mwezi Juni mwaka huu, utawala wa Aal-Khalifa ulimfutia uraia Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni mashuhuri na mkuu wa kimaanawi wa mapinduzi ya watu wa nchi hiyo suala ambalo lilikabiliana na radiamali kali kutoka ndani na nje ya nchi hiyo. Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al-Wifaaq nchini Bahrain ni shakhsia mwingine ambaye amekuwa akizuiliwa na vyombo vya Aal-Khalifa tangu mwezi Julai mwaka jana kwa tuhuma bandia dhidi yake. Kwa mujibu wa Adel al-Gharif mwanaharakati wa Bahrain, kamatakamata na dhulma zote zinazoshuhudiwa nchini Bahrain, zinasimamiwa kwa ukamilifu na idara ya ujasusi ya Saudia.