Kuendelea mashambulio ya Saudia nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1579-kuendelea_mashambulio_ya_saudia_nchini_yemen
Ndege za kivita za jeshi la Saudi Arabia, kwa mara nyingine tena zimefanya mashambulizi ya kikatili katika mji mkuu wa Yemen San'a na kuua kwa umati raia wa nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2016 02:29 UTC
  • Kuendelea mashambulio ya Saudia nchini Yemen

Ndege za kivita za jeshi la Saudi Arabia, kwa mara nyingine tena zimefanya mashambulizi ya kikatili katika mji mkuu wa Yemen San'a na kuua kwa umati raia wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Jana Ijumaa, ndege vamizi za Saudi Arabia zilifanya mashambulizi makubwa katika kijiji cha al Hawl mkoani San'a na kuua wakazi kadhaa wa kijiji hicho. Ndege za Saudia zilishambulia pia aneo la ar Rahidah mkoani Taiz, kusini magharibi mwa Yemen na kusababisha hasara kubwa za roho na mali za watu. Ndege za Saudia zilishambulia mara 20 nyumba za raia wa Yemen katika miji ya ar Rabua na al Baha katika eneo la mpakani mwa Yemen na Saudia na kuua raia kadha wa Yemen. Mwezi Machi mwaka jana Saudi Arabia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu na kwa baraka kamili za Marekani, ilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo kadhaa ya Yemen. Hadi hivi sasa maelfu ya raia wa Yemen wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameshauawa na maelfu ya wengine wamejeruhiwa. Vikosi vya wananchi wa Yemen kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo, jana viliendelea kujibu jinai za ukoo wa Aal Saudi kwa kushambulia maeneo ya kijeshi ya Saudia kwenye maeneo ya mpakani na kuangamiza wanajeshi kadhaa wa Saudi Arabia. Mashambulio ya kamati za wananchi wa Yemen kwenye maeneo ya kijeshi ya Saudia katika mpaka wa nchi hizo mbili yamewasababisha hasara kubwa Wasaudia. Kanali ya televisheni ya al Masira ya Yemen imetangaza habari ya kuangamizwa makubwa ya mamluki kutoka Pakistan wanaotumiwa na Saudia kufanya mauaji nchini Yemen. Mamluki hao wameangamizwa katika mkoa wa Hajjah wa magharibi mwa Yemen. Wakati huo huo mamluki wengine 23 walioivamia Yemen wameangamizwa katika mashambulizi ya jeshi na vikosi vya wananchi wa Yemen kwenye mkoa wa al Jouf wa kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo jana maelfu ya wananchi wa Yemen walifanya maandamano mjini San'a kulaani jinai za ukoo wa Aal Saud na za utawala wa Kizayuni na Marekani, na kusisitiza kuwa wataendelea kuilinda nchi yao mbele ya uvamizi wa maadui wa taifa lao. Nara kuu ya waandamanaji hao ilisema: "Kuiokomboa nchi yetu ni jukumu letu sote" na walisisitiza kuwa, maeneo yote ya nchi yao yanayokaliwa kwa mabavu na wavamizi hao, yatakombolewa. Waandamanaji hao kwa mara nyingine tena wametangaza kuliunga mkono jeshi na vikosi vya wananchi na kutaka kuendelea muqawama hadi pale kila shibri ya ardhi ya Yemen itakapokombolewa kutoka kwenye makucha machafu ya wavamizi. Wananchi hao wa Yemen wametaka pia wananchi wote wapewe mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kulinda nchi yao. Katika upande mwingine, wakuu wa makabila, vyama na wazee wa mkoa wa Ma'rib wa katikati mwa Yemen, jana Ijumaa walikutana mjini San'a kwenye kikao kilichoongozwa na mkuu wa mkoa huo Bw. Ahmad al Majidi na kusisitizia udharura wa wananchi wote kujitolea kukabiliana na wavamizi wa nchi yao. Wazee hao wa mkoa wa Ma'rib wamewataka wazee wa makabila mengine ya Yemen kusaidiana kwa ajili ya kukomboa ardhi za nchi hiyo. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, Yemen kamwe haiwezi kuwa tonge nyepesi kuimeza, na historia imethibitisha kuwa wananchi wa nchi hiyo hawajawahi hata mara moja kukubali kuwa chini ya wavamizi.