Sputnik: Kitabu cha mwongozo wa magaidi wa Syria kimechapishwa nchini Uturuki
Vikosi vya jeshi la Syria vimenasa nakala ya kitabu kilichochapishwa nchini Uturuki ambacho ndani yake kina maelezo ya utoaji mafunzo kwa magaidi kuhusu jinsi ya kutumia silaha za nyuklia.
Kitabu hicho kimegunduliwa na vikosi vya jeshi la Syria katika operesheni ya hivi karibuni ya kusafisha maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na magaidi katika mkoa wa Latakia kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Kitabu hicho cha mwongozo kilichoandikwa kwa lugha ya Kiarabu kiitwacho "Zadul- Mujahid" kimechapishwa mjini Istanbul, Uturuki na taasisi iliyochapa kitabu hicho haikuchukua hatua yoyote ya kuficha taarifa kuhusu asili yake.
Nembo ya mchapishaji wa kitabu na taarifa za kuwezesha kuwasiliana naye vimeorodheshwa pia kwenye kitabu hicho.
Askari wa jeshi la Syria aliyegundua kitabu hicho ameliambia shirika la habari la Sputnik kwamba ndani yake mumejaa maelezo ya kueneza chuki na kutoa mwito kwa watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka kupigana vita na wale wasio na itikadi sawa na yao.
Askari huyo aidha amebainisha kuwa ndani ya kitabu hicho kuna maelezo kuhusu kile kinachotajwa kuwa ni namna ya kuamiliana na "maadui na mali zao" .
Vilevile kitabu hicho cha "Zadul-Mujahid" kinazungumzia jinsi ya kuchoma moto miji iliyovamiwa na kushikiliwa na magaidi, kukata miti yake yote, kuharibu maisha ya watu na kuwaua wafungwa.
Kwa mujibu wa askari huyo wa Syria, ndani ya kitabu imeelezwa pia kuwa magaidi wanaweza kuwaoa mateka wao na hata kuweza kutumia silaha za nyuklia.
Tangu mwaka 2011 Syria imekuwa uwanja wa vita angamizi vilivyoanzishwa na magaidi wanaosaidiwa na kuungwa mkono na madola ya kiajinabi. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya watu laki nne wameuawa hadi sasa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.../