Raia saba Yemen wauawa katika hujuma za Saudia
Raia saba wameuawa katika hujuma ya hivi karibuni ya ndege za kivita za Saudia nchini Yemen.
Kwa mujibu wa taarifa raia hao wameuawa mapema leo Jumapili wakati ndege za Saudia zilipodondosha mabomu katika makazi ya raia katika mkoa wa Ibb kusini mwa Yemen.
Duru zinadokeza kuwa, idadi ya waliopoteza maisha inaweza kuongezeka kutokana na kuwa baadhi ya majeruhi wako katika hali mahututi.
Mapema, ndege za kivita za Saudia pia zilishambulia wilaya ya Kamaran na kituo cha Ndege za Kijeshi katika mkoa wa Hudaydah na Idara ya Kisiasa katika mkoa wa Sa'ada.
Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa Saudia na kuungwa mkono na Marekani umeshazishambulia skuli, hospitali, makaazi ya raia, misikiti, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo. Zaidi ya watu 10,000 wamepoteza maisha katika hujuma ya kinyama ya Saudia dhidi ya Yemen.
Lengo kuu la hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen ni kumrejesha madarakani kibaraka wake, Rais mtoro na aliyejiuzulu wa nchi hiyo Abd Rabu Mansour Hadi na kuwaondoa madarakani wanamapinduzi wa Ansarullah.