Wafanyakazi Saudia wafanya maandamano kwa kutolipwa mishahara yao miezi sita
Wafanyakazi wa moja ya mashirika makubwa ya eneo la mashariki mwa Saudia wamefanya maandamano kulalamikia kutolipwa misharahara yao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo wafanyakazi hao wamefanya maandamano hayo kulalamikia kitendo cha kutolipwa mishahara yao kwa miezi sita sasa. Wakati huo huo, Shirika la Kuchapisha Qur'ani nchini Saudia nalo limewafuta kazi wafanyakazi wake 1300 kwa kufilisika.
Wafanyakazi hao waliokuwa wakijishughulisha katika kituo kikubwa cha uchapishaji wa Qur'ani Tukufu cha Mfalme Fahdi huko mjini Madina, walikuwa hawajalipwa mishahara yao kwa kipindi cha miezi tisa kabla ya kufutwa kazini. Awali watu hao sanjari na kutakiwa kuwasiliana na idara ya uajiri ya Shirika la Oger la nchi hiyo, walitakiwa pia kusaini mkataba wa kuacha kazi.
Kushuka kwa bei ya mafuta, uungaji mkono kifedha kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri huko Saudia na Iraq na kadhalika vita vya muda mrefu nchini Yemen ambavyo hadi sasa vimeigharimu Saudia kiasi kikubwa cha fedha, ni mambo ambayo yameufanya utawala wa Aal-Saud, kukabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha. Hii ni katika hali ambayo, Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud ametoa amri ya kukatwa mishahara ya wafanyakazi wote wa serikali kwa ajili ya kuokoa bajeti ya serikali.
Itafahamika kuwa, Saudia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ukandamizaji wa wafanyakazi, na kwa mara kadhaa mashirika ya kutetea haki za binaadamu yamekuwa yakiilalamikia serikali ya kifalme ya nchi hiyo na kuitaka iheshimu haki za binaadamu.