Saudia yaendeleza mashambulio ya anga dhidi ya Yemen; raia kadhaa wauawa
Mashambulio ya anga ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika maeneo kadhaa ya Yemen yameua na kujeruhi raia kadhaa wa nchi hiyo.
Kanali ya televisheni ya Al-Mayadeen ya Lebanon imeripoti kuwa raia wasiopungua wanne wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio lililofanywa na ndege za kivita za Saudia hapo jana katika eneo la Adh-Dhai'ah kaskazini magharibi mwa Yemen.
Ndege za kivita za utawala wa Aal Saud zimeshambulia pia maeneo ya Athu'ban na Mandaba katika eneo la Baqam mkoani Sa'ada na vilevile mkoani Hajjah magharibi mwa Yemen.
Ndege za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia zimefanya mashambulio pia dhidi ya wilaya ya al-Mashjah mjini Sarwah mkoani Ma'rib katikati mwa Yemen.
Katika kujibu jinai na mashambulio ya kinyama yanayofanywa na ndege za Saudia, kikosi cha makombora cha jeshi la Yemen kikishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi kimefyatua makombora kadhaa dhidi ya kambi ya kijeshi ya Abul Madh na kituo cha Samit'ah katika eneo la Jizan kusini mwa Saudia.
Vikosi vya jeshi la Yemen vimeshambulia kwa makombora pia mkusanyiko wa wapiganaji mamluki wa Saudia kusini mwa mji wa Kahbub mkoani Lahj kusini mwa Yemen.../