UN yapinga kufanyika uchunguzi kuhusu jinai za Saudia huko Yemen
Umoja wa Mataifa umepinga suala la kufanyika uchunguzi kuhusu jinai na uhalifu unaofanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen.
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) limepinga kuanza uchunguzi huru kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na jinai zilizofanywa na Saudi Arabia dhidi ya raia huko Yemen na badala yake, baraza hilo limetaka kuundwe kamati ya kitaifa ili kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na pande zinazozozana huko Yemen hususan kuuliwa raia na kushambuliwa hospitali nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatua hiyo ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imevunja matumaini ya wanaharakati wa haki za binadamu ambao wao pamoja na Zeid Ra'ad bin al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, walikuwa wametaka kufanyike uchunguzi huru kuhusu mashambulizi ya anga ya muungano vamizi wa Saudi Arabia huko Yemen.
Siku kadhaa zilizopita Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa katika Kituo cha Utafiti wa Haki za Binadamu huko Cairo, Misri kuwa, Saudi Arabia na nchi waitifaki wake kama Marekani hadi sasa zimeonyesha kuwa zinaweza kuzuia kufanyika juhudi za Umoja wa Mataifa za kuwawajibisha wahusika wa jinai za kivita huko Yemen.