Saudia yaacha kutumia kalenda ya Kiislamu na kuanza kutumia ya Kikristo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i16609-saudia_yaacha_kutumia_kalenda_ya_kiislamu_na_kuanza_kutumia_ya_kikristo
Saudi Arabia imetangaza kuacha kutumia kalenda ya Kiislamu ya Hijria Qamaria na kuanza kutumia kalenda ya Kikristo katika kazi za kiserikali kutokana na kile ilichosema ni sehemu ya kubana matumizi.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Oct 03, 2016 11:40 UTC
  • Saudia yaacha kutumia kalenda ya Kiislamu na kuanza kutumia ya Kikristo

Saudi Arabia imetangaza kuacha kutumia kalenda ya Kiislamu ya Hijria Qamaria na kuanza kutumia kalenda ya Kikristo katika kazi za kiserikali kutokana na kile ilichosema ni sehemu ya kubana matumizi.

Saudia ilianza kutumia Kalenda ya Kiislamu mwaka 1932 lakini mashirika ya mafuta yamekuwa yakitumia Kalenda ya Kikristo ya Gregorian kufanya biashara  na kulipa mishahara.

Kalenda ya Kiislamu ya Hijria Qamaria ina miezi 12 yenye siku 354 au 355, yaani siku 11 chache zaidi ya Kalenda ya Kikristo. Mishahara Saudia inahesbiwa kwa mwaka na hivyo mwaka mrefu zaidi utamaanisha kazi zaidi na mshahara mdogo kwa wafanyakazi. Kalenda ya Kikristo imeanza kutumika Saudia Jumapili ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya mwaka 1437 Hijria Qamaria.

Sarafu ya Saudia inazidi kuporomoka thamani

Mabadliko hayo ni kati ya hatua za kubana matumizi ambazo zimechukuliwa na utawala wa kifalme Saudia kutokana na kupungua bei ya mafuta ghafi ya petroli katika masoko ya kimataifa. Aidha Saudia imepata hasara kubwa kutokana na oparesheni zake za kijeshi nchini Yemen ambapo sasa imekwama katika kinamasi baada ya kushindwa kufikia malengo yake tokea ianzishe hujuma Machi 2015. Saudia pia imewakatia mishahara na marupurupu wafanyakazi wa serikali wakiwemo mawaziri ili kubana matumizi. Halikadhalika Saudia imeongeza bei ya umeme, maji na huduma zingine za serikali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa ruzuku.

Duru zinasema Saudia inakabiliwa na nakisi ya bajeti ya takribani Dola bilioni 100 jambo ambalo limepelekea watawala wa ukoo wa Aal Saud kuingiwa na wasiwasi mkubwa.