Saudia yapinga kuundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu jinai ilizofanya Yemen
Utawala wa Saudi Arabia umepinga wito wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kutafuta ukweli kuhusu jinai zilizofanywa na utawala huo nchini Yemen.
Utawala wa Riyadh umetangaza msimamo huo mwishoni mwa kikao cha kila wiki cha baraza lake la mawaziri.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein ametoa wito wa kuundwa tume huru ya kimataifa ya kufanya uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Saudia nchini Yemen.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch nayo pia yamelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lisimamishe uanachama wa utawala wa Aal Saud katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo hadi utakapokomesha mashambulio yake dhidi ya Yemen.
Amnesty International aidha imezitaka serikali za Uingereza na Marekani zisimamishe uuzaji silaha kwa utawala wa Riyadh.
Itakumbukwa kuwa hapo kabla Umoja wa Mataifa uliiweka Saudia kwenye jalada lake jeusi kutokana na jinai na mauaji ya watoto iliyofanya nchini Yemen lakini baadaye ilibadilisha uamuzi wake kutokana na mashinikizo ya utawala huo wa Aal Saud.
Tangu mwezi Machi 2015, Saudi Arabia, kwa kushirikiana na baadhi ya nchi nyingine za Kiarabu za Mashariki ya Kati pamoja na Marekani zimeanzisha mashambulio makubwa dhidi ya Yemen kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake, Rais mtoro na aliyejiuzulu wa nchi hiyo Abd Rabu Mansour Hadi na kuwaondoa madarakani wanamapinduzi wa Ansarullah.
Zaidi ya watu 10,000 wameshapoteza maisha katika hujuma ya kinyama ya Saudia dhidi ya Yemen, wakiwemo wanawake na watoto wadogo. Mbali na kuua raia wasio na hatia mashambulio hayo yamelenga na kuteketeza pia skuli, hospitali, makaazi ya raia, misikiti, barabara, masoko na kambi za wakimbizi.../