Saudia: Hatutachunguza jinai tulizofanya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i16822-saudia_hatutachunguza_jinai_tulizofanya_yemen
Kwa mara nyingine tena Saudi Arabia imepinga wito wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kutafuta ukweli kuhusu jinai zilizofanywa na utawala huo nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 06, 2016 01:10 UTC
  • Saudia: Hatutachunguza jinai tulizofanya Yemen

Kwa mara nyingine tena Saudi Arabia imepinga wito wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kutafuta ukweli kuhusu jinai zilizofanywa na utawala huo nchini Yemen.

Adel Bin Zayd al-Tarifi, Waziri wa Utamaduni na Vyombo vya Habari wa Saudi Arabia amesema Riyadh haiko tayari kutekeleza wito wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein anayetaka kuundwa tume huru ya kimataifa ya kufanya uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Saudia nchini Yemen.

Akizungumza jana Jumatano, al-Tafiri alisema Saudia haikubaliani na takwa hilo kwa kuwa tayari Riyadh ilikubali uchunguzi unaofanywa na Kamisheni ya Taifa ya Yemen, ambayo inaripoti moja kwa moja kwa Abd Rabbuh Mansur Hadi, rais mtoro na aliyejiuzulu wa Yemen.

Athari za hujuma za kinyama za Saudia nchini Yemen

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch nayo pia yamelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lisimamishe uanachama wa utawala wa Aal Saud katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo hadi utakapokomesha mashambulio yake dhidi ya Yemen.

Zaidi ya watu 10,000 wameshapoteza maisha katika hujuma ya kinyama ya Saudia dhidi ya Yemen tangu Machi mwaka jana 2015, wakiwemo wanawake na watoto wadogo.