Kuongezeka uungaji mkono wa Marekani kwa magaidi wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17173-kuongezeka_uungaji_mkono_wa_marekani_kwa_magaidi_wa_syria
Duru za habari zimeripoti kuwa, baada ya dola la kibeberu la Marekani kuwapatia magaidi wa Syria makombora ya Grad, hivi sasa Washington imeyapa magenge hayo makombora ya kutungulia ndege ya kubeba begani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2016 03:11 UTC
  • Kuongezeka uungaji mkono wa Marekani kwa magaidi wa Syria

Duru za habari zimeripoti kuwa, baada ya dola la kibeberu la Marekani kuwapatia magaidi wa Syria makombora ya Grad, hivi sasa Washington imeyapa magenge hayo makombora ya kutungulia ndege ya kubeba begani.

Gazeti la Saudia la al Sharq al Awsat na ambalo ni maarufu kwa kuyaunga mkono magenge ya kigaidi nchini Syria limemnukuu mtaalamu mmoja wa Marekani katika masuala ya Syria akisema kuwa, shehena zisizopungua mbili za makombora hayo ya Marekani yamefikishiwa magenge yenye silaha kaskazini mwa Syria.

Mtaalamu huyo Mmarekani aidha amesema, makombora ya Kimarekani aina ya TOW nayo yanaelekea kwa waasi wa kaskazini mwa Syria hivi sasa. Amesema, makombora ya Grad yaliyoko mikononi mwa magaidi wa Syria yana uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 20 hadi 40 na kuongeza kuwa, Marekani imeyapa magenge hayo ya kigaidi makombora hayo ili yashambulie maeneo ya wanajeshi wa Syria.

Naye Rami Abdul Rahman, mkuu wa kundi la haki za binadamu lenye mfungamano wa karibu na wapinzani wa Syria amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, makombora hayo ambayo Marekani imeyapa magenge ya kigaidi, yako tayari kwa ajili ya kushambulia maeneo ya wanajeshi wa Syria.

Makombora ya Marekani yako mikononi mwa magenge ya kigaidi yanayofanya jinai nchini Syria na Iraq

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, hatua hiyo ya Marekani ya kuwapa waasi makombora ya kisasa, haina lengo jengine ila kujaribu kulidhoofisha jeshi na serikali ya Syria, na kuyatia nguvu magenge ya kigaidi. Hivyo madai yote yanayotolewa na Marekani ya kwamba ina hamu ya kuona mapigano yanakomeshwa nchini Syria, hayana msingi wowote.

 

Jambo lililo wazi ni kuwa, katika wiki za hivi karibuni, serikali ya Syria imepata ushindi mkubwa katika mapambano yake dhidi ya magenge ya kigaidi na hivi sasa jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi, limekaribia kuwamaliza magaidi wanaoungwa mkono na madola ya kibeberu hususan Marekani. Hivyo viongozi wa Washington wanatumia hila na ujanja wa kila namna ili kuzuia kuangamizwa kikamilifu magenge ya kigaidi nchini Syria. Mara zote Marekani imekuwa ikija na mapendekezo ya kusimamishwa mapigano kila pale inapoona magaidi wameelemewa huko Syria na mara zote Washington imekuwa ya mwanzo kukanyaga ahadi zake za kusimamisha mapigano.

Magaidi wanaodaiwa na Marekani kuwa ni wenye misimamo ya wastani wanachinja kama kuku hata watoto wadogo wagonjwa nchini Syria

 

Ni hivi karibuni tu ambapo Marekani ilitangaza kukata mazungumzo yote na Russia kuhusiana na usimamishaji vita licha ya nchi hizo mbili kukubaliana kusimamisha vita nchini Syria na kuruhusu misaada ya kibinadamu iwafikie raia waliokwama katikati ya mapigano. Hivi sasa pia Marekani imetangaza hadharani kuwa imewapa makombora mapya magaidi wa Syria na shabaha yake kuu ni kushambulia maeneo ya jeshi la nchi hiyo.

Hatua hiyo inahesabiwa na weledi wa mambo kuwa ni tafsiri ya kivitendo ya matamshi ya hivi karibuni ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliyodai kuwa itachukua hatua za upande mmoja za kijeshi kuamiliana na mgogoro wa Syria. Uamuzi huo wa White House wa kutumia zaidi chaguo la kijeshi katika mgogoro wa Syria umechukuliwa katika hali ambayo, magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya kigeni yanayoongozwa na Marekani hayajawaletea tija yoyote wananchi wa Syria ghairi ya uharibifu mkubwa, kuuliwa watu wasio na hatia, kuwa wakimbizi wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu na kukosekana utulivu katika kipindi chote hiki cha miaka sita sasa ya uadui linaofanyiwa taifa la Syria. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ni jambo lisilo na shaka kwamba, mgogoro wa Syria ni tata mno, lakini tatizo kuu la mgogoro huo ni uingiliaji wa madola ya kigeni, kupewa fedha na silaha magenge ya kigaidi na kuendelea kumiminwa magaidi ndani ya ardhi ya Syria kutoka kona mbalimbali za duniani ambapo Marekani ina nafasi kubwa na ya kimsingi katika jinai zote hizo.