Magaidi wa Kiwahabi washambulia shule Syria, waua wanafunzi
Magaidi wa Kiwahabi wamefanya shambulio dhidi ya shule moja kusini mwa Syria na kuua watoto kadhaa waliokuwa darasani.
Televisheni ya serikali ya Syria imetangaza kuwa, magaidi wameshambulia kwa makombora kadhaa shule ya eneo la Lis'har katika mkoa wa Daraa, kusini mwa nchi hiyo ambapo kwa akali watoto watano wameuawa na wengine 15 kujeruhiwa vibaya.
Wakati huo huo juhudi za magenge ya kigaidi za kutaka kuyadhibiti maeneo ya mkoa wa Lattakia, magharibi mwa Syria, zimezimwa na weledi wa jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na muqawama wa wananchi.
Katika operesheni hiyo, askari watatu wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa, huku makumi ya magaidi wakiangamizwa. Kadhalika jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa mji wa Kawkab katika viunga vya mkoa wa Hama, magharibi mwa nchi hiyo kutoka mikononi mwa magaidi wakufurishaji.
Wakati huo huo, mapigano makali yameibuka baina ya makundi mawili ya kigaidi yanayojiita "Ahraru sh-Sham" na "Jundul-Aqsa" katika mkoa wa Idlib, magharibi mwa Syria. Katika mapigano hayo makumi ya magaidi wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.