HRW yakosoa ukiukaji wa haki za binadamu Saudia
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limekosoa ukiujaki wa haki za binadamu unaofanywa nchini Saudi Arabia. Shirika hilo limekosoa bikali utolewaji wa hukumu na adhabu kali dhidi ya wapinzani na vile vile kuendelea kushikiliwa kizuizini makumi ya wanaharakati wa haki za binadamu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Mtandao wa habari wa al-A'had wa nchini Lebanon umelinukuu Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch na kuripoti kuwa, ripoti ya kila mwaka ya shirika hilo inaonesha kuweko ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia ambapo katika mwaka uliopita wa 2015 kuna wapinzani wengi ambao wamehukumiwa adhabu nzito jela na hata wengine kutekelezwa adhabu ya kifo dhidi yao akiwemo Sheikh Nimr Baqir al-Nimr mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo aliyekuwa akipigania haki za raia.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mara kwa mara kumekuwa kukiripotiwa ukiukaji wa haki za wafanyakazi wa kigeni wanaofanya kazi nchini Saudi Arabia ambao wamekuwa wakilazimishwa kufanya kazi masaa 18 kwa siku bila ya mapumziko, vilevile kunyimwa haki ya kurejea makwao hadi pale watakaporuhusiwa na waajiri wao.
Inaelezwa kuwa, mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Saudi Arabia nayo yamekuwa yakiikosoa serikali ya Riyadh kwa kuwakandamiza wafanyakazi wa kigeni.