UN yawasilisha mpango wa kuunusuru mji wa Aleppo, Syria
Mshauri wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa huko Syria amesema kuwa umoja huo umewasilisha mpango wenye vipengee vinne kwa ajili ya kuunusuru mji wa Aleppo kutoka katika udhibiti wa magaidi.
Jan Egeland amesema kuwa mpango huo wa Umoja wa Mataifa unajumuisha kutolewa zana na suhula za kitiba, kupelekwa wafanyakazi wa sekta ya afya na matibabu, utolewaji wa misaada ya chakula na vifaa vingine vya dharura na misaada ya kibinadamu huko Aleppo na uwezekano wa kuondolewa wagonjwa 300 wanaohitaji misaada ya kitiba huko mashariki mwa mji huo wakiambatana na familia zao.
Makundi ya kigaidi hivi sasa yamezingirwa na jeshi la Syria katika maeneo tofauti huko mashariki mwa mji wa Aleppo. Makundi hayo ya magaidi yanaendelea kuvurumisha makombora katika maeneo ya magharibi na yale yenye utulivu katika mji huo.
Magaidi hao pia wamewazuia raia wa maeneo ya mashariki mwa mji kuondoka katika maeneo hayo na sasa wanawatumia raia hao kama ngao za binadamu katika maeneo ya vita.