HAMAS: Tumejizatiti kwa makombora kukabiliana na chokochoko za Israel
(last modified Tue, 15 Nov 2016 15:02:48 GMT )
Nov 15, 2016 15:02 UTC
  • HAMAS: Tumejizatiti kwa makombora kukabiliana na chokochoko za Israel

Mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, ameelezea uwezo wa makombora iliyonayo harakati hiyo kwa ajili ya kutoa jibu kwa hujuma tarajiwa ya utawala haramu wa Israel.

Mushir al-Masri amesisitiza kuwa, hatua ya harakati hiyo ya muqawama kuwa na maelfu ya makombora, inaifanya iwe tayari kukabiliana na aina yoyote ya hujuma tarajiwa ya Israel.

Kombora la HAMAS

Ameongeza kuwa, kusalimu amri utawala haramu wa Kizayuni ndiyo njia pekee mbele ya muqawama na kwamba, harakati hiyo inao uwezo wa kutoa jibu kwa Israel kama ilivyofanya katika vita vya mwaka 2012 na 2014. Mjumbe huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, ameashiria juhudi za makundi ya wanamapambano kwa ajili ya kuachiliwa huru mateka wa Palestina wanaoendelea kushikiliwa katika jela za kutisha za utawala huo bandia na kusisitiza kuwa, harakati hiyo kamwe haitorudi nyuma kunako misimamo yake. Hadi sasa karibu wafungwa elfu sita wa Kipalestina wanaendelea kushikiliwa na utawala pandikizi wa Israel huku, 750 kati yao wakiwa hawajafunguliwa mashtaka.

Baadhi ya wanamapambano wa Palestina

Aidha Mushir al-Masri amezungumzia njama za Israel za kupiga marufuku adhana katika misikiti ya mji wa Quds na kusema, kuadhiniwa katika mji wa al-Aqsa na misikiti mingine ya mji huo, kutaendelea na kwamba wale ambao wanakerwa na kunadi huko kwa ajili ya swala wanaweza kuhamia eneo jingine mbali na mahala hapo. Jumapili iliyopita, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, sauti ya adhana inasababisha udhia kwa baadhi ya walowezi wa Kiyahudi na hivyo ukaamua kupasisha muswada wa kupigwa adhana katika misikiti yote ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (yaani Israel).