Italia: Tuna matumaini mgogoro wa Syria utatatuliwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesema kuwa, ana matumaini njia za kidiplomasia zitautatua mgogoro wa Syria.
Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo kutoka mjini Rome na kumnukuu Paolo Gentiloni akisema hayo jana mwishoni mwa kongamano la pili la mazungumzumzo ya Meditteranean na kuelezea matumaini yake kuwa katika siku zijazo kutashuhudiwa dalili za kuanza mazungumzo baina ya John Kerry na Sergey Lavrov, mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Russia kuhusiana na Syria na njia za kuwafikishia misaada ya kibinadamu wakazi wa mashariki mwa Halab.
Gentiloni ameongeza kuwa, mazungumzo hayo yanaweza kuwa utangulizi wa kuanza mazungumzo yenye matunda mazuri yatakayoendeshwa na Stephen Demistora, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika suala la Syria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesema, haipasi kuruhusu eneo la Meditterranean likumbwe na machafuko na ni kwa sababu hiyo ndio maana nchi za eneo hilo zina wajibu wa kufanya jitihada kubwa za kutatua zenyewe matatizo yao.
Ripoti zinaonesha kuwa, takriban watu laki tatu wameshauawa, mamia ya maelfu ya wengine wamekuwa wakimbizi na taasisi za Syria zimeshapata hasara ya mabilioni ya dola, tangu ulipoanza mgogoro wa nchi hiyo karibu miaka sita iliyopita uliotokana na uingiliaji wa madola ya kigeni hasa ya Magharibi kama Marekani na ya kieneo kama vile Saudia, Qatar na Uturuki na kupelekea magenge ya kigaidi kuivamia nchi hiyo ya Kiarabu na kufanya mauaji dhidi ya raia na maafisa wa serikali.