Assad: Wamagharibi wanawapa himaya magaidi na sio raia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21439-assad_wamagharibi_wanawapa_himaya_magaidi_na_sio_raia
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema serikali za nchi za Magharibi zinawapa himaya na kuwakingia kifua magaidi wanaofanya jinai nchini humo na wala hazijali hali ya raia wa kawaida wa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-05T12:50:29+00:00 )
Dec 15, 2016 04:22 UTC
  • Assad: Wamagharibi wanawapa himaya magaidi na sio raia

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema serikali za nchi za Magharibi zinawapa himaya na kuwakingia kifua magaidi wanaofanya jinai nchini humo na wala hazijali hali ya raia wa kawaida wa nchi hiyo.

Katika mahojiano na shirika la habari la Russia Today hapo jana, Rais Assad amesema Wamagharibi hawajali wakati ambapo magaidi wanaua raia na wanaposhambulia turathi za kitaifa katika maeneo mbali mbali kama mji wa Palmyra, ambao umetekwa tena kwa mara ya pili na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na kubwa wanachojali, ni magaidi wanaowaunga mkono.

Amesema serikali za nchi za Magharibi zimeingiwa na kiwewe kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana na jeshi la Syria likishirikiana na wapiganaji wa kujitolea kwa upande mmoja na Russia kwa upande wa pili, katika mji wa Aleppo.

Wananchi wakisherehekea kukombolewa Aleppo

Amesema vyombo vya habari vya Magharibi vimekataa kuakisia kwa kina na kwa njia nzuri ushindi mkubwa wa taifa la Syria dhidi ya magaidi katika mji huo muhimu, ambao ulikuwa moja ya ngome muhimu za magenge ya kigaidi.

Hapo jana Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisema kuwa, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, raia zaidi ya elfu 6 wameuhama mji wa Aleppo na kupelekwa katika maeneo salama.

Aidha ripoti ya wizara hiyo imesema magaidi karibu 400 waliokuwa katika mji huo wameweka silaha chini na kujisalimisha. Mji wa Aleppo uliopo kaskazini mwa Syria umekuwa chini ya magenge ya kigaidi tokea mwaka 2011.