Wanajeshi wa Israel wamuua shahidi kijana Mpalestina huko Ramallah
Kijana mmoja Mpalestina ameuawa shahidi katika hujuma ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Taarifa zinasema, katika hujuma ya wanajeshi wa Kizayuni huko Ramallah Jumamosi alasiri , Ahmed Hazem Rimawi, kijana Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 19 aliuawa shahidi.
Rimawi ameuawa shahidi katika siku ambayo Wapalestina waliwazika mashahidi sita waliouawa katika mapambano ya Intifadha na wanajeshi wa Kizayuni. Miili ya Wapalestina hao ambao wameuawa katika kipindi cha miezi kadhaa sasa ilikuwa ikishikiliwa kinyume cha sheria na utawala wa Kizayuni. Tokea Intifahda (mwamko) mpya ya Quds ilipoanza Oktoba 2015 hadi sasa, Wapalestina 268 wameuawa shahidi.
Wakati huo huo, Brigedi ya Izzedin Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Hamas, ilitoa taarifa Jumamosi na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina. Brigedi hiyo imesema itajibu jinai hizo kwa kuongeza oparesheni zake dhidi ya Wazayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel.