Mkuu wa vyombo vya mahakama: Shahidi Raisi alijitolea kuwatumikia wananchi
-
Shahidi, Ebrahim Raisi
Mkuu wa vyombo vya Mahakama vya Iran anasema kuwa Rais Shahidi Ebrahim Raisi alijitolea kwa dhati kuwatumikia wananchi na kusabilia maisha yake kwa ajili ya Iran.
Katika ujumbe aliotuma katika mtandao wa kijamii, Gholamhossein Mohseni Ejei amemuenzi na kuashiria kutimia mwaka wa pili wa tangu kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi na maafisa kadhaa wa serikali na kueleza kuwa: Mbinu ya Shahidi Raisi ya kuwazingatia wananchi ilikuwa sehemu ya msingi ya akhlaqi na mtindo wake wa usimamizi.
Ameongeza kuwa, Shahidi Raisi alikuwa muwazi kikamilifu katika kueleza misimamo ya kimapinduzi na kiitikadi, kubainisha fikra za Mapinduzi ya Kiislamu katika vikao mbalimbali bila ya kusita.
Ejei amekumbusha kuwa, Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Mapinduzi ya Kiislamu alimsifu Raisi kwa kuwajali wananchi, kwa kusabilia maisha yake kuwatumikia wananchi bila kuchoka, aidha alimsifu kwa Uchamungu na hekima; akizitaja sifa zake hizo kuwa nishani ya juu kabisa ya heshima.
Raisi alitumikia mfumo wa Kiislamu na kuwatumikia wananchi wa Iran kwa miaka mingi katika nyadhifa mbalimbali ndani ya mahakama, akiwa Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran.
Mkuu wa vyombo vya Mahakama vya Iran pia amempongeza mwendazake Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian. Amesema, Amir- Abdollahian alikuwa mwanadiplomasia stadi na mwanamapinduzi ambaye, kama alivyokuwa Rais Raisi, alifanya juhudi kubwa kueleza misimamo ya kimapinduzi na kujenga daraja kati ya medani ya vita na diplomasia.