Saudia: Marekani haijapunguza mauzo ya silaha zake kwetu
Adel al-Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amekanusha madai kuwa Marekani imepunguza kiwango cha uuzaji silaha kwa serikali ya Riyadh kutokana na hujuma za utawala huo wa kifalme nchini Yemen.
Jubeir ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari pambizoni mwa mwenzake wa Marekani, John Kerry mjini Riyadh na kubainisha kuwa, utawala huo wa Aal-Saud haujapokea taarifa yoyote kutoka Washington kuhusu kuangalia upya muamala wao wa mauzo ya silaha.
Amesema hizo ni propaganda za vyombo vya habari na kusisitiza kuwa Saudia karibuni hivi itapokea shehena ya mabomu erevu (Smart Bombs) kutoka Marekani.
Wakati huo huo John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema serikali ya Washington inafanya kila iwezalo kuona kuwa mauzo yake ya silaha kwa Riyadh yanaimarika siku baada ya siku.
Hii ni katika hali ambayo, mapema mwezi huu, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kwa mara nyingine tena lilitoa wito kwa Marekani kusitisha uuzaji wake wa silaha kwa Saudi Arabia. Katika barua kwa rais anayeondoka wa Marekani Barack Obama, mkuu wa HRW mjini Washington, Sara Margon, pia aliitaka Marekani iache kuwatuma askari wake kushiriki katika hujuma zilizo kinyume cha sheria katika nchi ya Yemen.
Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia na kuungwa mkono na Marekani mbali na kuua raia zaidi ya 11,000 wasio na hatia, umeshazishambulia na kuharibu kimamilifu asilimia kubwa ya skuli, hospitali, makaazi ya raia, misikiti, barabara, masoko na kambi za wakimbizi katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.