Hivi ndivyo Uingereza inavyochochea jinai Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i23335-hivi_ndivyo_uingereza_inavyochochea_jinai_mashariki_ya_kati
Wakati kuna kila dalili zinazoonesha kuwa, Uingereza inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inarejea katika Ghuba ya Uajemi, ushahidi mpya umethibitisha kwamba mkoloni huyo mkongwe wa Ulaya anahusika moja kwa moja katika jinai zinazofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 12, 2017 07:32 UTC
  • Hivi ndivyo Uingereza inavyochochea jinai Mashariki ya Kati

Wakati kuna kila dalili zinazoonesha kuwa, Uingereza inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inarejea katika Ghuba ya Uajemi, ushahidi mpya umethibitisha kwamba mkoloni huyo mkongwe wa Ulaya anahusika moja kwa moja katika jinai zinazofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia.

Baada ya Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza na Boris Johnson, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, David Cameron, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza amekuwa mtu wa tatu wa nchi hiyo kuitembelea Bahrain na kuonana na viongozi wa nchi hiyo ndogo ya Kiarabu katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, safari hizo za mfululizo za viongozi wa Uingereza nchini Bahrain zimesababishwa na hali iliyopo hivi sasa katika nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Nchi hizo hivi sasa zinajaribu kuligeuza baraza hilo kuwa umoja, lakini hitilafu kubwa zilizopo baina yao zinazuia kutekelezwa ndoto hiyo. Miongoni mwa vizuizi vikubwa vya kufikiwa njozi hiyo ni migogoro ya mipaka iliyopo baina ya nchi hizo kama vile mgogoro wa mpaka baina ya Qatar na Imarati na mgogoro wa mafuta baina ya Saudi Arabia na Kuwait, migogoro ambayo imepunguza kiwango cha maelewano ya nchi hizo katika kipindi cha hivi karibuni. Migogoro mingine iliiyopo baina ya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ni mzozo kuhusu nafasi ya kila nchi katika masuala ya eneo hili. Inaonekana kuwa nchi za Imarati na Qatar zinataka kupunguza ushawishi wa Saudi Arabia kwenye baraza hilo. Jambo jengine ambalo linaonekana lina mchango katika kutofanikiwa ruya ya kulibadilisha baraza hilo kuwa umoja ni msimamo unaooneshwa wazi na Marekani ambayo inaonekana haitaki tena kujiingiza sana katika masuala ya Ghuba ya Uajemi.

Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza akiwa na Wafalme wa Saudi Arabia na Bahrain

 

Ni jambo lisilo na shaka hata chembe kwamba mkoloni kizee Uingereza anataka kurejea kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi. Ukweli wa jambo hilo uko wazi kama mbaramwezi. Ni katika miezi ya hivi karibuni tu yaani mwishoni mwa mwezi Oktoba 2016, ambapo Uingereza ilifungua kituo cha jeshi lake la majini nchini Bahrain. Bila ya shaka yoyote hatua hiyo ilihitajia sababu ya kuihalalisha na kama tunavyojua, UIngereza ni bingwa wa siasa za tenganisha watu uwatawale. Isingeliwezekana hata kidogo kwa mkoloni huyo khabithi kuachana na siasa zake hizo na ndio maana wakati wa kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi huko Bahrain, Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza hakuuzuia ulimi wake kutamka hadharani kuwa eti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni tishio kwa usalama wa nchi za Kiarabu. Nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi nazo zinaonekana kufurahia kurejea Uingereza kwenye eneo hili. Viongozi wa nchi hizo wanahisi wana deni kwa Uingereza kwani wanaamini ni siasa za Uingereza ndizo zilizoziweka madarakani tawala kama za ukoo wa Aal Khalifa na Ma-Aal wengine wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Tab'an kuweko madarakani tawala hizo za kiukoo kuna faida kubwa kwa madola ya Magharibi kwani kwa kisingizio cha kupata uungaji mkono katika masuala ya kiulinzi, nchi hizo za Kiarabu zinatoa gharama kubwa ya kuzilipa nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza na hivyo kuzipunguzia matatizo yao ya kiuchumi.

Uharibifu mkubwa unaofanywa na mabomu ya vishada yanayotumiwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen

 

Wakati tunaposema kuwa Uingereza ni mshirika wa jinai zinazotendeka Mashariki ya Kati huwa hatukuongeza chumvi. Siasa za kijeshi za miongo ya huko nyuma za Uingereza zimemfanya mkoloni huyo kuwa mshirika wa jinai zinazotendwa leo na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Ushrikiano la Ghuba ya Uajemi hususan Saudia. Ni hivi karibuni tu ambapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilifichua kuwa, katika muongo wa 1980, London iliiuzia Saudi Arabia mabomu 500 ya vishada, mabomu yaliyopigwa marufuku ambayo hivi sasa yanatumiwa na Saudi Arabia kuua wanawake, watoto na watu wasio na hatia huko nchini Yemen. Katika barua yake kwa mbunge mmoja muhafidhina anayejulikana kwa jina la Philip Hollobone, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Michael Fallon aliandika: Uingereza iliipatia Saudi Arabia mabomu 500 ya vishada aina ya BL 755 kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili yaliyotiwa saini mwaka 1986. Shehena ya mwisho ya mabomu hayo ilipatiwa Saudia mwaka 1989.