Quds ni mstari mwekundu kwa Waislamu wote
(last modified Fri, 20 Jan 2017 04:22:26 GMT )
Jan 20, 2017 04:22 UTC
  • Quds ni mstari mwekundu kwa Waislamu wote

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO amesisitiza kuwa mji mtakatifu wa Quds ni mstari mwekundu kwa Wapalestina, kwa ulimwengu wa Kiarabu, kwa Waislamu na pia kwa Wakristo ulimwenguni.

Shirika la habari la IRNA limenukuu Mahmoud Ismail akisema hayo jana kujibu mpango wa Marekani wa kutaka kuhamishia ubalozi wake katika mji wa Quds kutoka Tel Aviv na kuonya kuwa, hatua hiyo itaripua mambo duniani na kamwe Wapalestina hawako tayari kunyamazia kimya kuvunjiwa heshima mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas.

Amesema, viongozi wa Palestina wana msimamo usiotetereka kuhusiana na kufuatilia jinai za utawala wa Kizayuni katika vyombo vya kimataifa kwa kuonesha orodha ndefu ya jinai za Israel dhidi ya Wapalestina. 

Wakati huo huo, Sheikh Zaid Sallah, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina amesema, kama Donald Trump ataamua kuhamishia Quds ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv, hatua hiyo italeta maafa makubwa duniani.

Waislamu wa Palestina wakisali katika mji mtakatifu wa Quds

 

Amesema, uamuzi wa Trump wa kuuhamishia Quds ubalozi wa Marekani unakinzana na sheria za kimataifa kwamba kwa mujibu wa sheria hizo mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na Israel haukubaliani na mpango wowote wa Kizayuni.

Mkuu huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina aidha amelaani njama za Israel za kuuyahudisha mji wa Quds na kusema kuwa njama hizo zitashindwa tu kwamba utawala pandikizi wa Israel hauna chochote ndani na unaendelea kuporomoka.

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa Marekani, Donald Trump ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na jinai zake aliahidi kuuhamishia Quds ubalozi wa nchi hiyo iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani.

 

Tags