Kuendelea mapigano katika maeneo tofauti ya Yemen
Licha ya Umoja wa Mataifa kuonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Yemen kutokana na mashambulio yanayofanywa na kundi linalojiita muungano wa Waarabu unaoongozwa na Saudia, mashambulio ya anga na mizinga ya kundi hilo yangali yanaendelea kwenye kona mbalimbali za Yemen.
Televisheni ya al Masira ya nchini Yemen imeripoti kuwa, jana Alkhamisi ndege za kivita za Saudia na wenzake ziliendelea kufanya mashambulizi ya kikatili katika mkoa wa Lahaj wa kusini mwa nchi hiyo na kwenye maeneo tofauti ya mkoa wa San'a na ya kaskazini na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa upande wake, shirika la habari la Yemen limetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo na kamati za wananchi zimeendelea kupambana na askari vamizi wa Saudia kwenye maeneo tofauti yakiwemo maeneo ya mpakani ya mkoa wa Asir na hususan katika mji wa ar Rabua na kuwasababishia hasara kubwa askari hao vamizi. Wakati huo huo wanajeshi wa Yemen wamefanikiwa kuzima shambulio la wanajeshi vamizi wa Saudia katika eneo la Khanjar la mkoa wa al Juf wa kaskazini mwa nchi hiyo baada ya kuua makumi ya mamluki wa Saudia akiwemo kamanda wa kikosi kilichojaribu kupenya kwenye eneo hilo. Habari nyingine zinasema kuwa, makabila ya Yemen yameitisha kongamano kubwa mjini San'a na kwa mara nyingine yametangaza uungaji mkono wao kwa jeshi na wanamapambano wa Ansarullah wanaopigania kukomboa ardhi za nchi hiyo zilizotekwa na wanajeshi wa nchi vamizi zinazoongozwa na Saudi Arabia. Bw. Muhammad Yahya al Ghuli, mmoja wa wakuu wa makabila ya mjini San'a amesema, kongamano hilo la jana lilisitizia wajibu wa kushikamana kikamilifu na muqawama wa jeshi na wananchi wa Yemen hadi watakapowafurusha mamluki wa Saudia katika kila shibri ya ardhi ya Yemen. Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen nayo imetoa tamko ikitangaza kuwa, mashambulio ya anga ya Saudia na wenzake katika bandari kuu za Yemen, yameongeza orodha ya jinai za kila siku za Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen na kuitaka jamii ya kimataifa ilaani jinai na mzingiro wa kidhulma pamoja na hasara kubwa za roho na mali zinazosababishwa na Saudi Arabia nchini humo. Kamati hiyo imeonya pia kuhusu madhara ya mashambulizi ya mtawalia katika bandari ya al Hudaidah na kusisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kuishambulia tu bandari hiyo ni jinai ya kivita kabla ya hata kufikiria mauaji ya watu wasio na hatia yanayofanywa na Saudia kwenye mashambulizi yake hayo. Katika upande mwingine, Jamie McGoldrick, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amesema kuwa, mamilioni ya wananchi wa Yemen wanahitajia misaada ya dharura na kuitaka jamii ya kimataifa kufanya haraka kuwasaidia wananchi hao. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, licha ya kupita karibu mwaka mmoja tangu Saudia ilipoanzisha mashambulizi ya kivamizi huko Yemen mwezi Machi 2015, lakini ukoo wa Aal Saud umeshindwa kufanikisha malengo yake. Ushahidi wa wazi wa suala hilo ni kuwa, hadi hivi sasa Saudia imeshindwa kumrejesha madarakani Abdu Rabbuh Mansur Hadi, Rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu kwa hiari yake na kukimbia nchi. Hadi hivi sasa zaidi ya watu elfu nane wameshauawa na 16 elfu wengine kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi katika mashambulizi hayo ya kikatili ya Saudia na wenzake nchini Yemen.