Jan 27, 2017 07:20 UTC
  • Lebanon yataka kutatuliwa mgogoro wa Syria kwa njia za amani

Rais wa Lebanon amesisitiza kuwa mgogoro wa Syria unapasa kupatiwa ufumbuzi kwa njia za amani na kisiasa.

Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema kuwa nchi yake inataka mgogoro wa Syria utapatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani na kwamba Beirut inaamini kuwa hiyo ni njia pekee sahihi ya kuhitimisha vita na tatizo la wakimbizi wa Syria.

Rais wa Lebanon aliyasema hayo jana katika mazungumzo yake na Bi Federica Mogherini ambaye ni Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya katika Ikulu ya Baabda mjini Beirut. 

Bi Federica Mogherini akiwa na Rais Michel Aoun wa Lebanon katika Ikulu ya Baabda mjini Beirut 

Rais Aoun pia amesisitiza kuwa uchaguzi wa Bunge wa Lebanon utafanyika kama ilivyopangwa yaani mwezi Mei mwaka huu na kwamba kutajitokeza mlingano kati ya makundi mbalimbali bungeni iwapo uchaguzi huo utafanyika.

Kwa upande wake Bi Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya pia ameshukuru misaada inayotolewa na Lebanon kwa wakimbizi wa Syria na kueleza kuwa, Umoja wa Ulaya utazidisha misaada inayohitajika kwa taasisi rasmi za Lebanon zinazohusika na wakimbizi.

Bi Mogherini pia amemwalika Rais wa Lebanon kuyatembelea makao makuu ya Umoja wa Ulaya na kuzungumza na viongozi wa umoja huo huko Brussels, Ubelgiji. 

Tags