Ansarullah: Saudia imeshindwa kufikia malengo yake haramu Yemen
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imesema utawala wa kifalme wa Aal-Saud umeshindwa kupata natija katika mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu na jirani yake.
Hayo yamesemwa na kiongozi wa Ansarullah, Abdul-Malik Badreddin al-Houthi katika hotuba ya jana, kwa mnasa wa miaka miwili tangu Saudi Arabia iivamie Yemen na kuanzisha mashambulizi ya anga ya kila siku.
Al-Houthi amesisitiza kuwa, licha ya Riyadh na waitifaki wake kutumia silaha za maangamizi dhidi ya raia wa Yemen, lakini wananchi hao wamesimama kidete na kusimama pamoja dhidi ya utawala huo wa kifalme.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni, jumuiya za kimataifa zikiwemo za International Solidarity, Care, Madaktari Wasio na Mipaka na Action Against Hunger zilitangaza katika kikao kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa kwamba mgogoro wa Yemen unaelekea kuwa moja kati ya migogoro mikubwa zaidi ya wanadamu katika dunia ya sasa.

Saudia ikisaidiwa na Marekani na waitifaki wake wengine walianzisha hujuma za kila upande dhidi ya Yemen tarehe 26 Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wao, Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen ambaye alijiuzulu nafasi hiyo na kukimbilia nchini Saudi Arabia.
Hata hivyo hujuma hizo hazijazaa matunda na badala yake, kwa mujibu wa Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Masuala ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, zimeua zaidi ya raia elfu 11, kujeruhi wengine 40,000 mbali na kuharibu asilimia kubwa ya miundomsingi ya nchi hiyo maskini.