Mar 09, 2016 08:02 UTC
  • Mchambuzi wa US: Saudia inaelekea kukumbwa na mgogoro wa kifedha

Mchambuzi mashuhuri wa masuala ya siasa wa Marekani amesema Saudi Arabia karibuni hivi itatumbukia katika mgogoro mkubwa wa kifedha.

James Savage ameliambia shirika la habari la Tasnim kuwa, utawala wa Aal-Saud unaedesha bajeti yenye nakisi kubwa kupita kiasi ya asilimia 15 hadi 20 ya mapato jumla ya taifa na kwamba kisima chake cha fedha kinaelekea kukauka. Savage amesema Shirika la Fedha Duniani IMF linakadiria kuwa utawala wa kifalme wa Saudia katika kipindi cha miaka mitano ijayo, utajikuta katika lindi la madeni na mgogoro mkubwa wa kifedha.

Wakati huo huo, mchambuzi huo ambaye ni Profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Virginia nchini Marekani amesema kuwa, kufuatia kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, nchi hii ipo katika njia ya kustawi tena kiuchumi na kurejea katika nafasi yake katika uchumi wa dunia. Amesema kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja nchini Iran unatazamiwa kupindukia dola bilioni 3 za Marekani kwa mwaka. Ameongeza kuwa, zaidi ya dola bilioni 58 za Iran ambazo zilikuwa zimezuiwa na serikali pamoja na mabenki ya nje, sasa zitakabidhiwa nchi hii.

Tags