Marekani yakiri imeua raia 400 Syria na Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27196-marekani_yakiri_imeua_raia_400_syria_na_iraq
Muungano unaodaiwa ni wa kupambana na genge la kigaidi la Daesh unaoongozwa na Marekani umekiri kwamba katika kipindi cha baina ya mwaka 2014 hadi 2017 umeua karibu raia 400 nchini Iraq na Syria katika mashambulizi yake ya anga.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 03, 2017 04:37 UTC
  • Marekani yakiri imeua raia 400 Syria na Iraq

Muungano unaodaiwa ni wa kupambana na genge la kigaidi la Daesh unaoongozwa na Marekani umekiri kwamba katika kipindi cha baina ya mwaka 2014 hadi 2017 umeua karibu raia 400 nchini Iraq na Syria katika mashambulizi yake ya anga.

Mtandao wa habari wa al Mas'ala wa nchini Iraq uliripoti habari hiyo jana (Jumapili) na kuinukuu komandi kuu ya operesheni za kijeshi ya muungano huo unaoongozwa na Marekani ikisema katika taarifa yake kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwezi Agosti 2014 hadi februari 2017, muungano huo umefanya mashambulizi 18,600 ya anga na kwamba raia waliouawa kwenye shambulizi hayo ni karibuni 396.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, tangu ilipoanza operesheni ya ukombozi wa Mosulu mwezi Oktoba 2016 hadi uliopokombolewa kikamilifu upande wa mashariki wa mji huo tarehe 18 Februari mwaka huu, kumeripotiwa matukio 37 ambayo kuna uwezekano raia wamekuwa wahanga wa mashambulizi ya muungano huo huku matukio 15 kati ya hayo yakithibitishwa kuuuliwa raia ndani yake.

Raia ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya Marekani na genge la Daesh katika nchi za Syria na Iraq

 

Hata hivyo, takwimu rasmi zinazotolewa na muungano huo unaoongozwa na Marekani ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi kubwa ya raia wanaouawa kila leo kwenye mashambulizi ya anga ya Marekani na waitifaki wake huko Syria na Iraq.

Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria iliwatumia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo likiwataka watekeleze majukumu yao ya kuwalinda raia wa nchi hiyo wanaouliwa ovyo na muungano unaoongozwa na Marekani.

Serikali ya Syria inasema, unachofanya muungano huo wa Marekani ni kushambulia raia na miundombinu ya nchi hiyo na si kupambana na magaidi.