Jumuiya za haki za binadamu: Mjumbe wa UN amefeli Yemen
Jumuiya na mashirika ya kutetea haki za binadamu yametangaza katika mkutano uliofanyika Paris nchini Ufaransa kwamba Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Ismail Ould Sheikh ameshindwa kutekeleza majukumu yake.
Mwenyekiti wa Muungano wa Kimataifa wa Kutetea Haki za Binadamu na Uhuru, Muhammad al Shami amesema Ismail Ould Sheikh hajui jinsi ya kukabiliana na hali mbaya ya watu wa Yemen na mazingira ya kisiasa ya nchi hiyo.
Naye Lauren Suri ambaye ni afisa wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mpaka amekosoa misimamo iliyodhidi ya Yemen ya baadhi ya nchi na kusema, nchi hizo hazitaki kusema na kudhihirisha ukweli wa mambo huko Yemen kutokana na kushirikiana kwao na Saudi Arabia na kuiuzia silaha nchi hiyo.
Wakati huo huo Julian Dosar wa Shirika la Madaktari Duniani amekosoa mtazamo wa jamii ya kimataifa kuhusu yanayojiri nchini Yemen na kusema: Mgogoro wa Yemen umepuuzwa kutokana na propaganda za vyombo vya habari juu ya vita vya Syria na Iraq.
Mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia na washirika wake walianzisha mashambulizi makali dhidi ya watu wa Yemen kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wao, Abdrabbuh Mansur Hadi aliyetoroka nchi na kukimbilia Riyadh. Ripoti zinasema maelfu ya raia wa Yemen wameuawa hadi sasa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.