Wasiwasi wa Umoja wa Mataifa kwa jinai za Saudia nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i2776-wasiwasi_wa_umoja_wa_mataifa_kwa_jinai_za_saudia_nchini_yemen
Raia watatu wa Yemen wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi ya jana Jumatano ya ndege za muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia kwenye maeneo ya makazi ya raia katika mkoa wa al Jawf, kaskazini mwa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2016 03:56 UTC
  • Mabaki ya baadhi ya silaha zilizopigwa marufuku zinazotumiwa na Saudia katika mashambulizi yake nchini Yemen.
    Mabaki ya baadhi ya silaha zilizopigwa marufuku zinazotumiwa na Saudia katika mashambulizi yake nchini Yemen.

Raia watatu wa Yemen wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi ya jana Jumatano ya ndege za muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia kwenye maeneo ya makazi ya raia katika mkoa wa al Jawf, kaskazini mwa Yemen.

Ndege za kijeshi za Saudia zilifanya mashambulizi pia katika mikoa ya al Bayda' na Taiz ya kusini mwa Yemen. Umoja wa Mataifa na Wizara ya Afya ya Yemen zimetangaza kuwa, zaidi ya raia elfu nane wa Yemen wameshauawa hadi hivi sasa katika mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia nchini humo yaliyoanza mwezi Machi mwaka jana. Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR nalo limetangaza kuwa, watu milioni mbili la laki nne na 30,173 wamelazimika kukimbia makazi yao nchini Yemen kutokana na mashambulizi ya muungano huo vamizi. Shirika la UNHCR limetangaza kuwa, kuna idadi kubwa ya wakimbizi wa Yemen waliokimbilia maeneo mengine ya nchi hiyo, na wanaishi katika mazingira magumu sana ya mashambulizi ya mfululizo ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia. Kwa mujibu wa shirika hilo, hadi hivi sasa hakuna matumaini yoyote ya kutatuliwa kisiasa mgogoro wa Yemen ulioshadidishwa na uvamizi wa Saudia. Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa, idadi ya raia wa Yemen waliokimbilia maeneo yenye mapigano kama vile Taiz, Hajjah, San'a, 'Amran na Saada imeongezeka sana. Taarifa ya UNHCR imeendelea kusema, sehemu kubwa ya wananchi wa Yemen wamelazimika kuhama makazi yao wakiwa mikono mitupu na kukimbilia kwenye maeneo kama vile ya shule, majengo ya serikali na majengo yaliyohamwa wao na familia zao. Wakati huo huo Abu Malik al Fishi, mjumbe wa Kamati ya Mapinduzi ya harakati ya wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, harakati hiyo inaunga mkono mazungumzo ya kuutatua mgogoro wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, iwapo kutafikiwa makubaliano ya kusimamisha vita na Saudia, wahasirika wakuu watakuwa ni wale wale mamluki ambao wameshirikiana na Saudia kufanya jinai nchini Yemen. Vile vile amezungumzia njama za maadui za kufikia makubaliano ya kusimamisha vita huku mashambulizi ya Saudia yakiendelea na kusema kwamba jambo hilo halikubaliki kabisa. Habari zinasema kuwa mashambulizi ya kikatili ya Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen yanaendelea ili kuzipotosha fikra za walio wengi na kujaribu kuficha uhakika kwamba muungano vamizi unaoongozwa na Saudia kwa baraka kamili za Magharibi hususan Marekani na Wazayuni umeshindwa kukabiliana na harakati ya wananchi ya Ansarullah, na hadi leo umeshindwa kumrejesha madarakani mamluki Abdu Rabuh Mansour Hadi huko Yemen. Hii ni katika hali ambayo wapenda haki na watu wenye fikra huru kote ulimwenguni wanaendelea kulaani jinai za ukoo wa Aal Saudi nchini Yemen. Kundi la Badr katika Bunge la Iraq limeilaumu jamii ya kimataifa kwa kunyamazia kimya jinai hizo. Mkuu wa kundi hilo Qassim al A'raji ametoa tamko la kulaani kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya jinai hizo. Mkuu wa kundi hilo ameilamumu vikali Marekani kwa misimamo yake ya kindumilakuwili kuhusiana na matukio ya Mashariki ya Kati na kuitaka jamii ya kimataifa itekeleze majukumu yake kuhusu wananchi wanaoendelea kudhululimwa wa Yemen na ifanye juhudi zake zote kuhakikisha kuwa jinai za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen, unakomeshwa mara moja.