Waziri wa Lebanon: Iran ni mfano wa kuigwa wa demokrasia duniani
Waziri wa Fedha wa Lebanon Ali Hassan Khalili amesema uchaguzi nchini Iran ni miongoni mwa mifano bora ya kuigwa ya chaguzi za kidemokrasia zinazofanyika kwa uwazi zaidi duniani.
Khalil ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA ambapo mbali na kusisitiza juu ya ulazima wa kufuata mfano wa uchaguzi wa Iran kama moja ya mifano ya kuigwa ya chaguzi za kidemokrasia zenye mizizi na zinazofanyika kwa uwazi zaidi duniani, amesema, hali hiyo inaonyesha harakati na uendelevu lilionao taifa la Iran.
Waziri wa Fedha wa Lebanon ameongeza kuwa hakuna nchi yoyote ya Kiislamu, Kiarabu na nyenginezo duniani ambayo chaguzi zake zina sifa hizo zinazoshuhudiwa katika chaguzi zinazofanyika nchini Iran, ambazo licha ya kufanyika kwa utulivu na bila ya makuu zinashuhudia ushiriki mkubwa zaidi wa wananchi.
Ali Hassan Khalili, ambaye pia ni mjumbe wa harakati ya Amal nchini Lebanon amebainisha kuwa kigezo cha kuigwa kisicho na kifani cha uchaguzi wa Iran kinapaswa kuendelezwa pia katika nchi nyenginezo, kwa sababu katika chaguzi hizo zinajitokeza sura mpya za wanasiasa wanaoamini uwepo wa mzunguko wa kupokezana madaraka, huku usimamizi na ufatiliaji wa utendaji wa viongozi ukiwa unafanyika kwa namna bora kabisa.
Uchaguzi wa 12 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utafanyika Ijumaa ijayo ya tarehe 19 Mei sambamba na ule wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji.
Uchaguzi wa rais ambao upigaji kura wake utafanyika ndani na nje ya nchi utawachuanisha Rais Hassan Rouhani anayetetea kiti chake, Makamu wa Kwanza wa Rais, Es'haq Jahangiri, Meya wa Jiji la Tehran, Mohammad Baqer Qalibaf, mjumbe wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu, Mostafa Aqa-Mirsalim, Msimamizi wa Haram ya Imam Ridha AS, Sayyid Ebrahim Raeisi na Makamu wa Zamani wa Rais wa Iran, Mostafa Hashemi-Taba.../