Wanajeshi wa Israel wawaua shahidi vijana wanne Wapalestina
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewapiga risasi na kuwaua vijana wanne Wapalestina.
Kwa mujibu wa televisheni ya Al Mayadeen, vijana kadhaa Wapalestina Ijumaa alasiri waliwavamia kwa visu wanajeshi wa Kizayuni na kukabiliana nao katika Mlango wa Babul Amud wa Msikiti wa Al Aqsa, katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu. Katika makabiliano hayo vijana Wapalestina walimuangamiza mwanajeshi mmoja wa kike wa utawala wa Kizayuni na kuwajeruhi wengine wawili.
Katika makabiliano hayo, vijana wanne Wapalestina walipigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.
Kufuatia tukio hilo, utawala wa Kizayuni umeimarisha doria zake za kidhalimu katika njia zote zinazoelekea katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds.
Aidha siku ya Ijumaa, wanajeshi wa utawala haramu wa Israel walivamia maandamano ya amani ya kila wiki ya Wapalestina katika kijiji cha Kafr Qaddum katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Watu kadhaa walijeruhiwa katika maandamano hayo ambayo hufanyika kupinga ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Katika upande mwingine, kanali ya televisheni ya Al Alam nayo imeripoti kujeruhiwa Wapalestina kadhaa ambao walishambuliwa na wanajeshi wa Israel mashariki mwa Ukanda wa Ghaza.