Haider al-Abadi: Ukurasa wa Daesh mjini Mosul umefungwa
Saa chache baada ya kuenea habari juu ya kushindwa kikamilifu magaidi wa Daesh (ISIS) katika ngome yao ya mwisho kwenye maeneo ya mji mkongwe wa Mosul, Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi amesema kuwa, muda wa kutangazwa kukombolewa kikamilifu mji huo umekaribia na faili la Daesh limefungwa nchini Iraq.
Haider al-Abadi amesema kuwa, muda wa kutangazwa rasmi kukombolewa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa (Nineveh) umekaribia mno na hadi sasa jeshi la Iraq linadhibiti sehemu kubwa ya mji huo ispokuwa eneo dogo sana lililobakia.
Akiashiria mwendelezo wa mapambano makali ya jeshi la Iraq katika vita dhidi ya ugaidi wa Daesh kwemue maeneo tofauti ya Iraq, Al-Abadi amewataka wananchi wa nchi hiyo wasubiri habari nzuri za ushindi mkubwa wa jeshi la nchi hiyo ndani ya kipindi hiki cha likizo za sikukuu ya Idul-Fitr. Ameongeza kuwa, Daesh kwa sasa wanavuta pumzi ya mwisho nchini Iraq na sasa wanajaribu kufanya mauaji ya raia sambamba na kuwasababishia hasara kubwa raia hao.
Usiku wa jana, jenerali wa jeshi la Iraq, Abdul Ghani al Assadi alinukuliwa akisema kuwa, oparesheni ya kukomboa kikamilifu mji wa Mosul kutoka katika makucha ya magaidi wakufurishaji wa Daesh itamalizika siku chache zijazo na kwamba kwa sasa magaidi hao wamebaki katika eneo dogo sana la mji mkongwe wa Mosrul kwenye makazi ya raia.