Video: Daesh wasambaratishwa kikamilifu Iraq, ndoto ya ISIS yayeyuka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31124-video_daesh_wasambaratishwa_kikamilifu_iraq_ndoto_ya_isis_yayeyuka
Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi ametangaza kusambaratishwa dola la uongo la Daesh nchini humo, baada ya vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi kukomboa maeneo yote ya Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa. Tangazo hilo la Waziri Mkuu wa Iraq limekuja baada ya vikosi vya nchi kuukomboa msikiti mkuu na mkongwe wa al Nuri, katikati ya mji wa Mosul.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 29, 2017 10:52 UTC

Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi ametangaza kusambaratishwa dola la uongo la Daesh nchini humo, baada ya vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi kukomboa maeneo yote ya Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa. Tangazo hilo la Waziri Mkuu wa Iraq limekuja baada ya vikosi vya nchi kuukomboa msikiti mkuu na mkongwe wa al Nuri, katikati ya mji wa Mosul.

Kabla ya hapo pia, televisheni ya serikali ya Iraq ilikuwa imetangaza kusambaratishwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) katika ngome yake ya mwisho mjini Mosul, kaskazini mwa Iraq na hivyo kufuta ndoto ya magaidi hao wakufurishaji ya kuunda utawala wao Iraq na Syria.

Baada ya jeshi la Iraq kukomboa msikiti mkuu wa al Nuri mjini Mosul, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo imetangaza kuwa hivi sasa hakuna eneo lolote la Mosul lililobakia mkononi mwa Daesh.

Mnara wa msikiti wa al Nuri uliotumiwa na kiongozi wa Daesh kutangaza dola lake la Iraq na Sham. Siku chache zilizopita magaidi wa Daesh wameuripua kwa mabomu msikiti huo baada ya kuona vikosi vya Iraq vimekaribia mno kuukomboa

Luteni Jenerali  Abdul Amir Abdur Rashid Yar Allah, kamanda wa operesheni ya ukombozi wa mkoa wa Nainawa nchini Iraq amesema kuwa, maeneo yote yaliyokuwa yanashikiliwa na magaidi wa Daesh yamekombolewa.

Hata hivyo duru mbalimbali za Iraq zimesema kuwa, ingawa genge la kigaidi la ISIS halimiliki tena sehemu yoyote ile nchini Iraq, lakini hilo halina maana ya kumalizika kikamilifu mashambulizi na operesheni dhidi ya magaidi hao.

Itakumbukwa kuwa mwezi Juni 2014, Abubakar al Baghdadi, mkuu wa genge la wakufurishaji la Daesh alitumia mimbar ya msikiti huo mkongwe uliokombolewa leo, kutangaza dola lake la Iraq na Sham.

Msikiti huo wa al Nuri ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa magaidi wa Daesh na ndio maana umekuwa sehemu ya mwisho kukombolewa na jeshi la Iraq.

Wakazi wa Nainawa Iraq wakisherehekea ushindi

Habari nyingine zinasema kuwa, baadhi ya magaidi wa Daesh wamekimbilia na kujificha katikati ya raia katika maeneo ya kusini mwa Mosul, suala ambalo linawaongezeka kazi askari wa Iraq kutokana na kuhofia roho za raia wasio na hatia.

Katika upande mwingine, duru za kijasusi za Iraq zimetangaza kuwa zimeanza kumsaili Ziyad al Zawi (?) maarufu kwa jina la kamanda wa kemikali wa ISIS.

Opereseheni ya kuukomboa mkoa wa Nainawa wa kaskazini mwa Iraq ilianza mwezi Oktoba mwaka jana.