Baada ya kutangazwa kuuawa kiongozi wa Daesh, wanachama wake wamalizana
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31646-baada_ya_kutangazwa_kuuawa_kiongozi_wa_daesh_wanachama_wake_wamalizana
Baada ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kutangaza kifo cha mkuu wake Ibrahim al Samarrai, maarufu kwa jina la Abu Bakr al Baghdadi, kumezuka mapigano baina ya wafuasi wa al Baghdadi na wapinzani wake ndani ya genge hilo katika mji wa Tal Afar, magharibi mwa Mosul kaskazini mwa Iraq. Wafuasi kadhaa wa Abubakar al Baghdadi wametiwa mbaroni na mahasimu wao.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jul 11, 2017 23:34 UTC
  • Baada ya kutangazwa kuuawa kiongozi wa Daesh, wanachama wake wamalizana

Baada ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kutangaza kifo cha mkuu wake Ibrahim al Samarrai, maarufu kwa jina la Abu Bakr al Baghdadi, kumezuka mapigano baina ya wafuasi wa al Baghdadi na wapinzani wake ndani ya genge hilo katika mji wa Tal Afar, magharibi mwa Mosul kaskazini mwa Iraq. Wafuasi kadhaa wa Abubakar al Baghdadi wametiwa mbaroni na mahasimu wao.

Shirika la habari la IRNA jana Jumanne lilizinukuu duru za mkoa wa Nainawa zikisema kuwa, kumezuka uasi ndani ya kundi la wakufurishaji la Daesh katika mji wa Tal Afar, magharibi mwa Mosul kiasi kwamba wafuasi wa Abubakar al Baghdadi wametiwa mbaroni na wapinzani wao. 

Duru hizo zimeongeza kuwa, hivi sasa kundi la kigaidi la ISIS limeweka sheria ya kutotoka nje katika mji wa Tal Afar na wafuasi wa genge hilo wameparaganyika. Duru za kieneo za mkoa wa Nainawa zimeongeza kuwa, mabaki ya wafuasi wa Daesh katika mji wa Tal Afar wanagombana kuhusu mtu wa kumrithi Abubakar al Baghdad ambaye atakuwa kiongozi mpya wa kundi hilo la kigaidi.

 

Siku ya Jumapili, Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi, alitangaza kupitia Tweeter, habari ya kukombolewa mji wa Mosul na kushindwa genge la kigaidi la Daesh katika mji huo. Juzi Jumatatu alitangaza rasmi kwa njia ya televisheni, kukombolewa mji huo akiwa katikati ya eneo la kale la Mosul ambalo ndilo lililokuwa ngome kuu ya magaidi wa ISIS.

Kabla ya hapo televisheni ya al Alam ilikuwa imeunukuu mtandao wa habari wa al Sumaria News wa Iraq ukisema kuwa, hatua ya genge la ISIS ya kutangaza habari ya kuuawa kiongozi wake al Baghdadi katika mazingira ya kimya kana kwamba haina umuhimu wowote, imezusha maswali mengi kati ya wanachama wa genge hilo la kigaidi hususan kwa kuzingatia kuwa, habari za kuuawa viongozi wengine wa Daesh zimekuwa zikipewa umuhimu mkubwa na genge hilo.